Asalaam Aleiykum,
Fanyeni siku maalumu za kutoka pamoja, jaribu utakavoweza kumpunguzia mkeo shughuli za jikoni, ifanyeni nyumba yenu iwe kivutio cha Ibadah,jitahidini sana msiseme uongo, asije mmoja wenu akawashambulia wazee wa mwenzie, pia msitumie lugha ya hasira na ghadhabu baina yenu. Semeni maneno matamu, mwenzio akikuwekea chai usisahau ahsante, akikupa maji mtazame usoni umpe ahsante, akikupa chakula sema Bismillah kwa sauti, na ukimaliza sema Alhamdullillah kwa sauti ikisha mpe ahsante, mimina mapenzi kwa mkeo au mumeo hayo yatafanya ndoa yenu idumu maisha, jaribuni kuishi maisha ya kawaida wala msifanye kuyataka mambo makubwa msokua na uwezo nayo.
Someni Quraan pamoja, nyote wawili kila wakati muwe mumependeza ndani ya nyumba, usimseme mwenzio kwa marafiki zako, usimcheke mbele za watu au mbele za watoto.
Usimfanyie vitimbi mwenzio, akikosea jaribu kumfundisha mwenzio kwa ukimya na mapenzi, mpikie mwenzio vyakula vizuri, ukiona baada ya hayo yote mwenzio ana safari za nje za udanganyifu usimzonge kwa matusi, ukigundua labda ana mambo fulani huko nje basi jiepushe kukutana naye kimwili mpaka ajirekebishe, mimina mapenzi na huruma mpaka mwenzio ajute moyoni. Kila wakati omba Mollah wangu nidumishe mimi na mume wangu, Kiroho, Kimwili, na ki Akili, utudumishe katika ufalme wako. Napenda kukumbusha Mume au Mke asidanganyike na vivutio vya nje, kwani hivo unavoviona nje ni (Projection)yako una buni wewe mwenyewe kwenye akili yako, ndio maana unachoona wewe kizuri mwenzio anakipita bila hata ya kugeuza uso, ukimuona fulani mbaya mwenzio anamkamata mkono hadharani, basi elewa hayo yote unayo yaona nje yanatokana na Akili yako na hiyo (Shetani)rahisi kukuchezea, lakini jambo la Mke au Mume ni jambo la Rohoni ambalo linadumu daima na hususan mkizaa, mnaweza kutengana kimwili lakini kiroho daima mtakua ndugu au marafiki.
Hapo aya inamalizia "Bila ya shaka katika hayo zimo ishara kwa watu wenye kufikiri" Na wewe kuwa mmoja wao katika hao wenye kufikiri ukifanikiwa kuipata hiyo fikira nini kitatokezea?Quraan Zukhruuf-70"ٱدۡخُلُواْ ٱلۡجَنَّةَ أَنتُمۡ وَأَزۡوَٲجُكُمۡ تُحۡبَرُونَ"
"Ingieni Bustanini (Peponi)nyinyi na wake zenu, mtafurahishwa (Humo)" Hapo tena unarejea kule mwanzoni "Nimekuumbieni wake zenu kutokana na jinsi yenu""Ewe Nabii Adam a.s kaa wewe na Mkeo kwenye Bustani", na nyinyi sasa mnaambiwa ingieni kwenye hii pepo(Bustani) nini mtafanyiwa(Zukhruuf-71)
"يُطَافُ عَلَيۡہِم بِصِحَافٍ۬ مِّن ذَهَبٍ۬ وَأَكۡوَابٍ۬ۖ وَفِيهَا مَا تَشۡتَهِيهِ ٱلۡأَنفُسُ وَتَلَذُّ ٱلۡأَعۡيُنُۖ وَأَنتُمۡ فِيهَا خَـٰلِدُونَ"
"Watakuwa wanapitishiwa sahani za (Dhahabu)na vikombe vya (Dhahabu),na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele"
Fanya subira na mkeo au mumeo tulia ulee watoto wako, ewe ndugu yangu pata shida hapa duniani ili ukapate hivyo ambavyo nafsi inavipenda na macho inavifurahia, inayotakiwa hapo ni subira tu wala si chengine, usije ukakimbia familia yako na mkeo hapa duniani utakosa hapa ulimwenguni na kesho huko akhera, mwisho ukifanya kheri utalipwa kheri, na ukifanya shari utalipwa kwa shari yako.Mollah wetu zisitiri ndoa zetu na vizazi vyetu, wapatanishe walogombana,zisafishe nyoyo zetu uyajaze mapenzi yako, ikisha utukirimu sisi pepo yako ya milele.Amin
Abdulla Baja
No comments:
Post a Comment