Saturday, December 8, 2012

MAISHA YA KIDINI PART-2

Asalaam Aleiykum,

Vipi nitaziepuka nyayo za shetani ili nianze kuishi maisha ya kidini, nifanye nini hata namie nipate hazina hii ya kidini, vipi nibadilike kuelekea katika Maisha alo yaridhia Mollah wangu, sasa bora nijitizame nimeshaanza kubadilika kueleka kwenye huo ukamilifu wa hukumu, huwezi kufanya yote hayo mpaka kwanza hamaki ziondoke, huwezi kuishi maisha ya kidini ikiwa katika moyo wako kuna japo chembe ya chuki, jiulize jee mimi naweza kusamehe nikikosewa?Mbona nina wivu? kwanini nina hasira?mbona moyo wangu una husuda?mbona sipendi watu bure pasi na kosa lolote?kwanini maneno madogo tu yananifanya nigombane na mwenzangu maisha, Mbona mkali kwa mke wangu au mume wangu?, kwanini mpaka watoto wangu wananiogopa? Kumbuka matatizo yote haya yamo ndani ya nafsi yako, vitu hivi vyote vimo kifuani hapo aliposema Bwana Mtume s.a.w sasa (Taqwa)itakaa wapi?, vipi utaweza kuyapata maisha ya kidini, kuyapata maisha haya lazima kwanza ujisafishe, Kwani hapo kifuani mfano wake kama maji yaliyomo mtungini, na mtungi tunaujua ukiutingisha au kuutia kata basi maji yanatibuka na hali kama hiyo ndio inayotokea kwako wewe.
Maisha ya kidini ni magumu kwa sababu sote tunaishi nje ya kifua, kinyume na maagizo ya Bwana Mtume s.a.w, tuishi ndani ya kifua,  ndio maana tunakabiliwa na ugumu wa kuishi kidini kwa sababu sote tumo kwenye mashindano ya kila siku, lazima ujenge jumba la kifahari, lazima uwe na gari nzuri ya kumshinda fulani, huwezi kuwa na furaha mpaka utajirike, sasa kama una matamanio hayo yote ya nje unataka hichi na kile lazima uvipate vipi utayapata maisha ya kidini. Kifua chako kimejaa matakwa ya kidunia na huku unataka maisha ya kidini, hapo dini haiwezi kuingia ndio maana utaona Sala zote ni za kuonesha watu, kila kitu chako lazima watu wakishuhudie, ukisali peke yako unasoma sura fupi kisha huyo unakimbia lakini ngoja akugonge bega mtu huko nyuma yako unaweza kusoma nusu msahafu hujijui unamsalia Mungu au binaadamu.
Bwana Mtume s.a.w alipoashiria kifuani mwake mara tatu alitaka Umma wake urejee ndani, Ili kila mmoja apate kuishi maisha ya kidini, Maisha yenye kufuzu. Mpaka sasa hivi unasoma maisha yako na yangu sote tunaishi nje, awe Sheikh, au Mwanafunzi, Imam au Maamuma sote sawa bado hatujui vipi kuishi maisha ya kidini yaliyomo vifuani mwetu, na ukichunguza hakuna hata Mmoja mwenye furaha sote tumejishughulisha na kuchuma mali, tunafukuzia kutafuta pesa, Labda mtu maradhi yake umaarufu, wengine wanataka cheo ndio waridhike, mwengine ataka aonekane yeye mzuri, na Mbaya zaidi ni yule anotaka aonekane yeye Mcha Mungu, na wengine wanaweka shuruti lazima nipate kitu fulani ndio nitakua furahani, ukiwa na hali hizo na zengine mfano wa hizo basi jijue unaishi nje ya kifua chako. Ama yule alokua hana shuruti lolote lile na tayari kasharejea kwenye kifua chake huyu anakua kashaisoma aya hii.Endelea part 3

No comments:

Post a Comment