Sunday, December 30, 2012

SHEREHE ZA SIKU MPYA-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Anachotakiwa Muislam aliye Muumin wa kweli alojifunga na Mollah wake kwa dhati ya Imani basi sherehe yake itakua ya kila siku, na wala sio mwaka, katika maisha ya Muislam aliyekua macho kila siku ni sherehe kwake, akiamka kusali Alfajiri kwake ni siku mpya, jua linapochomoza kila kitu kinaamka na kuanza kutoa sauti, ndege wanaimba, mpaka jua lina raha zake likikuchoma, mpaka kuku wanazungumza lugha yao, kumbuka hakuna siku ilo fanana, kila siku ni tafauti na mwenzake.
Huoni tafauti jana ulikua unaumwa leo mzima, kitoto chako kimepiga hatua moja leo hii, mkeo jana kapika kile leo kapika hichi, leo asubuhi Asumini zimechanua, watoto wanakwenda school wamefurahi, mawingu jana yalikua meupe leo meusi, jana bahari ilikua imechafuka leo imetulia, jana nilisali msikiti fulani leo nasali na fulani, leo nimesikia sauti ya huyu jana nimesikia ya yule, paka wanagombana, jogoo anawika, hii ndio sherehe ya Muumin, hataki yeye mwaka mpya, kwake kila siku ni mpya na kila siku ni furaha, sababu yeye mwaka mzima yuko macho.
Na ukiwa utaziangalia hizo siku utagundua hazifanani kabisa, na kila siku ina mambo mapya, huna haja tena ya kusheherekea mwaka mpya kwani kwako wewe kila siku ni sherehe. Ila kama umelala ndio subiri December 31 ndio uamke kidogo ikisha ulale tena mpaka mwakani, lakini kama unataka sherehe ya Kiislam basi ipokee siku anayo kukirim Mollah wako, ipokee uienzi, angalia yote yanotokea kuanzia Alfajiri mpaka Magharib utaona pamejaa sherehe tupu, ndege wanashereheka,, vitoto vimefurahi, mpaka miti inashangiria. Na ukigundua hayo kuna siku pia itakuja utafunguliwa mengine na Mollah wako katika Rehma zake ili upate kuona mambo mepya katika ulimwengu huu unaoishi ambayo yapo lakini huyaoni kwa kuwa bado umelala, hebu tazama miujiza hii ili uione furaha ya maisha, hebu tazama ithbati hii umepewa nguzo tano na pia umeumbwa na vidole vitano haikujii chochote katika akili yako.
Hebu amka uifurahie siku na sio mwaka, hebu furahi sio kwa kujua vidole na nguzo tano tu bali na vyengine kama vitano hivi, hayo macho kupata kuona, masikio kupata kusikia, mikono yako kupata kugusa, pua yako kupata kunusa harufu, na ulimi kupata kujua ladha, hazitoshi kuwa sherehe za siku mpya juu yako, na ukisheherekea nguzo hizo tano basi utakua ni mwenye kushereheka na kila kitu katika maisha yako na wala husubiri mwaka mpya.
Nakutakieni kheri za siku mpya na furaha za kila siku.Namuomba Mollah atupe furaha za kila siku na tuzijue Rehma zake tunazo ziona na tusizo ziona Amin.

No comments:

Post a Comment