Asalaam Aleiykum,
Darsa yetu ya leo inaanza na kisa cha kasuku aliyekuwa anamilikiwa na mabibi wawili katika mji wa Kiislam, Kama ilivyo desturi ya Miji yetu dini nzima inakua mikononi mwa Sheikh, Dhana yetu inatupa yeye ndiye anayejua na yeye pekee ndie mteule wa kutukamatia mfumo mzima wa dini, na anachosema yeye hakina makosa ndani yake, vipi itakua na makosa wakati yeye kasoma vitabu, anajua hadith na akiisema hadith moja ndio inakua muongozo mzima wa dini unategemea hadith hiyo, hiyo ndio hali tulo nayo hivi sasa. Kumbuka hii ni hadith ya Kasuku na kama ilivyo hadith yaweza kuwa ya ukweli imetokea au ya uongo imetungwa, lakini upo kwenye darsa usizuke ukaanza kubaki kwenye hadith ukakosa mafundisho ndani ya hadith hiyo, kama yanafaa chukua na kama hayafai yaache ndani ya hadith hiyo, na ukifanya hivyo haitokudhuru chochote hadith hii.
Naam, Kama ilivyo Desturi ya sisi Masheikh tunapenda kufanyiwa Takrima za Ugeni, tunapenda (Mahanjumati)mialiko ndio maradhi yetu, sasa katika mji huu kulikuwa na hawa Mabibi wawili maskini wakipenda sana mambo ya dini na wakitaka kufanya japo machache yenye kheri wakaamua kumualika Sheikh wao, wakamuandalia hapa ndizi mbivu, machapati, sambusa ziko hapo , pale kuna mikate ya ufuta nk, takriban walijitahidi ili mgeni wao apate kufurahi, alipohudhuria yule Sheikh akawa anazunguka kwenye sahani zote ziloandaliwa na chakula kilikua kitamu mno, baada ya kumaliza akaomba dua na kuwaambia wale mabibi nimefurahi sana na chakula chenu na Insha Allah nitakua mwenye kuja kila Alkhamis kutia baraka kwenye nyumba hii. Ikawa ada ya Sheikh yule miezi nenda miezi rudi, na dua yake hiyo hiyo moja, Mungu akujaalieni afya, mzidi kupika vyakula vizuri zaidi.
Mwanaadamu ndio mwanaadamu wale Mabibi wakachoka na hali ile, na Mja akichoka ana aina mbili katika machaguzi ama atafanya visa, au atasimanga, wale mabibi wakaamua kusimanga miezi nenda miezi rudi, washamchoka Sheikh, akitoka wanatukana matusi yaso idadi, Sheikh gani, mroho mkubwa, anatupa dhiki, hatuna uwezo, dua yenyewe moja tu kama kameza keseti, na hivi na vile wakati wanasema haya Kasuku kakaa kimya anawasikiliza, walipogundua Kasuku atawakashifu wakafanya ada Sheikh kabla ya kuingia wanamfunika Kasuku. Siku moja ikatokezea Sheikh kasahau kitabu chake kinachoitwa (Mwenye kuyajua yalofichikana)ikabidi kabla ya kwenda Msikitini apite kwa wale mabibi ili akachukue kitabu chake, alipogonga Mlango, wale Mabibi moja kwa moja wakaufungua ikawa mbele yao kasimama Sheikh, wakawa hawana budi kumkaribisha ndani, alipoingia ndani baada ya kutoa salamu, Kasuku akasikia sauti ya Sheikh na mambo yakaanzia hapo, Kasuku akaanza kusema kila alokua anasikia, Mroho mkubwa, kazi kufakamia makatlesi na sambusa,Alkhamis haijafika umekuja tena, si Sheikh chochote, kusikia matusi ya kasuku yanazidi ikabidi kwa aibu wale mabibi wakimbilie jikoni, Sheikh kainamia chini, Kasuku akasema yote mpaka alipomaliza yale yalotiwa katika kichwani mwake kasuku akanyamaza, aliponyamaza Sheikh akachukua kitabu chake akatoka, waliposikia mlango umefungwa wale Mabibi wakatoka jikoni wakaja ukumbini, ikawa macho yao wao na kasuku wanatizamana, Kasuku akasema sasa nifunikeni.
Na hivi ndivo kila mmoja wetu anavoendelea na maisha yake, ama anajifunika mwenyewe au anaomba sasa nifunikeni, Usikubali ukawa maisha yako kama kasuku, Kasuku anasema alosikia, ndio maana wengine ukiwagusa (Hususan Wasomi) wanahamaki sana maana yake anajijua yeye ni Kasuku, kakusanya taaluma fulani ya kupatia maisha, baada ya hiyo taaluma ananyamaza kimya kama kasuku, na mimi nafanya hivi ili kuondosha kiburi, huwezi kuwa Mcha Mungu kama una kiburi, kwa hiyo napagusa kwenye hicho kisomo chako ili nikushushe tuwe sawa, nikutoe kwenye (Tundu la Kasuku)kwa hiyo usichukie ukafanya (Personal)ukasusa natumia nyezo katika nyenzo zangu nyingi za kuvunja (Viburi)Naam usikubali mwalimu wako akawa kasuku utakua hasarani, Usiishi maisha yako kama Kasuku ikawa wewe muigizaji, umeona watu wamefanya na wewe umefanya, mpaka dua zako zitizame unataka pesa lakini unasoma sura ya (Zilzal)unashida nyengine lakini unatumia Dua ilotungwa miaka 100 ilopita, basi wewe huna hata uwezo wakutunga dua yako ya kuomba, mpaka uwe kama Kasuku.
Sasa unajiuliza mimi niwe vipi, ukitaka kujua uwe vipi Endelea Part 2
Very Nice Story
ReplyDeleteits nice.....sheikh Abdallah...
ReplyDelete