Monday, April 1, 2013

MAKOSA YA MJA MWENYE SHIDA-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Kwa wale wanodhani mimi ni mtowaji mawaidha nawaomba wabadilishe dhana zao, na ukisoma Darsa zangu ukadhani ni mawaidha utakua mwenye kukosa faida na mafundisho yaliyomo katika darsa hizi. Mawaidha wajibu wake ni kitu cha kusikiliza, na kusikiliza kuna hiyari ama utasikia maneno au sauti, ukisikia maneno kidogo yatakushitua, yatakugusa japo kwa mbali, lakini ukisikia sauti ndio itakua mtoa mawaidha kasema kitu chengine na wewe unakuja na tafsiri  ya kitu chengine kabisa. Sasa nini kazi yangu mimi katika darsa hizi, Nia yangu ni kukupa nyenzo ya kuweza kukubadilisha na ukifahamu darsa hizi unakua mtu mwengine kabisa, Uislam wako na ufatiliaji wako wa mambo ya kidini unabadilika na kuwa wa vitendo sio wa maneno.
Basi leo pata faida ya Mja mwenye shida yaweza kuwa wewe au nikawa mie, Sote tuna shida na kwa vyovyote sote ni wenye kuhitaji, sasa nini kinacho tusib mpaka tukawa tunaingia matesoni, kipi kinacho tujulisha sasa tumeshazama matesoni, cha mwanzo kabisa kuondoka ni hiyo Imani ya uchache iliyomo kwenye mioyo yetu kupotea, na Imani ikipotea unakua umekitupa kitu kikubwa sana chenye thamani na wewe. Ndio maana utaona hata kitendo cha Sala   zetu zimejaa maombi matupu, japokua hiyo Sala ni maombi lakini kusudio lake sio kila ukenda kwa Mollah wako unasahau hata kumuabudu ila wewe mwenye kuomba cheo, au utajiri, labda mwanao apasi mtihani au jirani afilisike, hiyo ndio Sala yetu unaomba hiki unataka kile umesahau hata dhumuni la hiyo sala na umekwenda kwa Mollah wako kwa ajili ya kitu gani, unajisahau kabisa inakua unamaliza sala nzima imejaa pesa au fulani adhurike, na kama unakaidi haya wewe yachunguze maombi yako na utagundua kama haya nisemayo ni kweli, na ukishagundua kama haya nisemayo ni kweli basi piga kelele unusuriwe sababu umo hasarani.
Angalia vipi mtu anakua akiambiwa Sali sala za usiku utafanikiwa anakuaje, Unaweza wewe ulomwambia ukatoka mbio, anaweza Mja huyo akasali miezi sita sababu ya Shida yake itekelezwe, lakini Ole wake iwapo Mwenye-enzi-Mungu hajampa matakwa yake, subiri utizame manyago yatotendeka hapo, nini kinatokezea kama hakufanikiwa, machafuko gani Mja huyu anayafanya mpaka Malaika wanaogopa, hatari kubwa, anabadilika Mja huyu kwanza anakwenda kwa Masheikh labda wana miujiza au dua walizo zificha, na kama hapo haiwezekani sasa Mja huyu ndio anaanza vitimbi mara kalala na kisu au kafutika ndimu, safari za kwa waganga ndio zinakua nyingi kuliko hata Msikitini, hata akimbiwa anyoe kope za macho zinatolewa mara moja, ajifunge kitanzi alale nacho pia yuko tayari, Maskini Mja anakua kashaingia hasarani na kuendelea kutenda makosa makubwa kwa Mollah wake, hapo hata Usali na Sijida lichune uso unakua Muflis. Wewe ni mwenye kumshirikisha Mollah wako, na Mollah wako hayuko Radhi na wewe na unaendelea kuishi katika shida na wala hazitatuki.
Sasa kwanini yanatokezea haya, kwa sababu kila mmoja wetu jambo la kwanza anahitaji Utajiri, kila mmoja wetu anahitaji kilichozidi, kile alichopewa hakitoshi, kila mtu anapigana Jihad hii mpaka tunakwenda katika Makaburi yetu hakuna mapumziko na hakuna hata mmoja alofanikiwa, na katika kuyatenda hayo yote tunakua tushajidhuru nafsi zetu kwa madhara chungu nzima ya Ufisadi na Husda, Dhuluma na kumkera Mwenye-enzi-Mungu na viumbe wenzetu na huku hatujui kwanini tunateseka. Kinacho tutesa kikubwa cha kwanza ni kusahau au kutokujua Maumbile ya Ulimwengu huu na Maandiko yake au (Sheria), Na cha pili ni kuondokwa na Imani. Hapa itabidi mnipe nafasi nilizungumze moja baada ya jengine ili upate muangaza au uzinduzi wa fahamu ili usiteseke tena, upate kujua sheria ya mambo ya Ulimwengu huu au mpangilio wake. Kwanza kabisa napenda kukumbusha katika Ulimwengu huu hayo matatizo ndio Mtihani wenyewe, kwa kuwa umesahau ndio maana unaanza kupigana na hayo matatizo, napenda uelewe wewe huwezi kuyashinda matatizo, daima matatizo yatakuzidi nguvu na kukushinda, kwanini ikawa hivyo?.
Mwenye-enzi-Mungu anatwambia katika kitabu chake kitukufu maneno yaliyomo kwenye sura ya Baqarah aya ya 155.

"وَلَنَبۡلُوَنَّكُم بِشَىۡءٍ۬ مِّنَ ٱلۡخَوۡفِ وَٱلۡجُوعِ وَنَقۡصٍ۬ مِّنَ ٱلۡأَمۡوَٲلِ وَٱلۡأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٲتِ‌ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ "
"Tutakutieni katika misukosuko ya (Maisha nayo) Hofu na Njaa na Upungufu wa Mali na Watu na wa Matunda, (basi) na Wapashe habari njema wanaosubiri". Kutaka kujua vipi unadanganyika mpaka unaishia kutenda makosa ya dhanbi kubwa, na ikisha upate (Method-Trick) au njia ya kufanya ili utokane na mtihani huu Endelea-Part 2

No comments:

Post a Comment