Asalaam Aleiykum,
Unateseka kwa sababu huna (Trust) Imani ima dhaifu au haipo kabisa, mambo yako yote yanaanzia kwenye (Ulimi) na kuishia hapo hapo Ulimini, Hutaki kuamini kwamba Maisha ni (Inshaa Allah) Unaona siku zote mambo yanavobadilika leo unakua Tajiri kesho unafilisika, leo mzima kesho una maradhi, Jana ulikua hai kesho unaitwa Marehemu(Maisha hayana Gurantee)Na hiyo ndio Inshaa Allah yenyewe. Anoishi Maisha haya hategemei uhakika wa Akiba wala kupata cha zaidi, kila saa na dakika yeye ni mwenye kumtegemea Mollah wake, Anaishi kama maisha ya Ndege, kama maisha ya Mnyama porini, au kama samaki Baharini, hebu watizame vipi wanyama maisha yao yakoje, ukiyagundua maisha ya wanyama vipi wanaishi kwa Inshaa Allah pengine yatakufungua (akili)huenda ukapata hekima ukatambua kumbe mimi kama samaki au ndege, Na sote tumeumbwa katika Ulimwengu huu tunapita njia, sasa kwanini mimi nahangaika na samaki haangaiki na sote tunakula, sote tunalala, nini kimenifika mimi, ikikujia fikra kama hiyo basi utaona unaanza kupiga hodi katika Mlango wa Maisha ya Inshaa Allah.Endelea kujiuliza nani anawaruzuku, na wakiumwa nani anawaponesha na ukiendelea sana moja kwa moja utajikuta umetokezea kwenye Ukumbusho wa Nabii Ibrahim a.s anaitaja Inshaa Allah kama hivi, sura ya Ash- Shuara aya ya 78 mpaka 81
"ٱلَّذِى خَلَقَنِى فَهُوَ يَہۡدِينِ"
"Ambaye ameniumba na Yeye ananiongoza"
Hivyo ndio inavotakiwa Inshaa Allah, Uikubali (Qadar)yake, kwamba la mwanzo yeye ndio kakuumba, ikisha kama wewe msomi kumbuka yeye ndiye aliyekupa kufahamu, kama utajiri yeye ndie aliyekufungulia njia kiajabu ajabu, kama cheo yeye ndie alosababisha mpaka wewe ukawepo hapo, yeye ndie amuekaye amtakaye, na kumuondosha anayemtaka, yeye ndie anaekuongoza katika kila jambo, ila bado wewe hujashuka katika mji wa Imani moyoni mwako ukagundua hayo.
"وَٱلَّذِى هُوَ يُطۡعِمُنِى وَيَسۡقِينِ"
"Na Ambaye ananilisha na kuninywesha"
Papara zako ndio zenye kukutesa, kutaka cha ziada ndio kunakupa madhara, lakini ukitulia ukaamini kikweli basi utagundua kweli mimi Mollah wangu ndie ananilisha na kuninywesha, tena sio tu kukupa riziki, bali hata ukisha kukipika, jiulize nani anayeona ladha, nani anayejua chakula kitamu, yote hayo ni Uwezo wa Mwenye-enzi-Mungu, Yule ambaye unamuasi, Yule ambaye unamsahau, nini habari yako wewe Ukiumwa kidogo, huwezi kula wala kunywa, watu hawashughuliki na chakula wala maji ila wanahangaika na (Drip)mpige shindano, mnyweshe kwanguvu, nani leo atakupa uwezo wewe wa kula na kunywa, yote hayo yanatokea kwa Mollah wako, wewe huwezi kunyanyua hata kidole bila amri yake, imekuaje leo unayapa mgongo maisha alokujaalia ya Inshaa Allah.
"وَإِذَا مَرِضۡتُ فَهُوَ يَشۡفِينِ "
"Na ninaposhikwa na maradhi yeye ndiye Ananiponesha"
Hivi ndio kuikubali (Qadar)Ninaposhikwa na Maradhi yeye kashanitengenezea (System)Maalumu, mimi nina jeshi yakiingia maradhi katika hili jumba langu basi kuna walinzi wananyanyuka bila ya mimi kuwapa amri na huanza kunilinda, mimi nina (Mabodyguard)kama ndege anavopona hendi hospital na mimi vilevile ninao uwezo huo ikiwa nitakamatana nayo Maisha ya Inshaa Allah, lakini weye, Malaria mtu anapiga bao, kichwa mtu anakwenda kwa mzee Mdumilo(Jina la kubuni), sasa hata (Doctor)hataki tena, kachoka na (Ampicilin)anataka lazima apate dawa ya Babu, hivi ndivo dunia inavotutesa kwa kuyapuuza Maisha ya Inshaa Allah.
"وَٱلَّذِى يُمِيتُنِى ثُمَّ يُحۡيِينِ"
"Na Ambaye atanifisha ikisha Atanihuisha"
Na nakubali mie baada ya Uhai wa duniani Mollah wangu ataniondosha na(Kufa)ikisha (Atanifufua kwa mara nyengine)
Huko ndio kuishi Maisha ya Inshaa Allah, na kuishi Maisha haya unatakiwa kukaribisha kila kitu, ukija utajiri sawa, nikiwa maskini sawa, nikiwa mzima kheri, na nikumwa pia niko radhi, ukiridhia mwenendo huo daima utakua furahani na huko ndiko kuishi kwa ajili ya kumtegemea Mollah wako wakati wote, Unakua unamkumbuka Mollah wako leo nini kakupangia, nani umtumikie, wapi atakutuma, nini atakupa upate kukitoa, wakati wote unajiweka katika kuongozwa Mwenye enzi Mungu.
Endelea Part 3
No comments:
Post a Comment