Sunday, June 2, 2013

MARAFIKI WA PEPONI PART 2

Asalaam Aleiykum,

Katika kupata uchambuzi wa jambo hilo inakuaje mambo yote yashaandikwa, basi mimi sina haja ya kuogopa au kuchukua tahadhari, sasa mwanzo kabisa tazama (Mifano) hii michache halafu utajijibu wewe mwenyewe ili upate kuzingatia, (Kuzaliwa kwako, kufa kwako, kuvuta kwako pumzi, kulala na kuamka kwako,vipi unavokula nani anasaga chakula chako,fikira zako mbona zinakuja bila ya wewe kutarajia na mengi mengineyo ambayo utayachunguza mwenyewe)yanatokea mambo haya bila ya ridhaa yako, kwa hiyo utaona kuna mambo una mamlaka nayo na kuna mambo huna mamlaka nayo, yale ulokua na mamlaka nayo hayo ndio utahukumiwa kutokana na matendo yake ima yawe mazuri au mabaya utalipwa kutokana na kadir ya uzito wake, Na hiyo ndio maana ya kuandikwa kabla ya hapo, Ama hili la kukutana na mwenzio hili liko katika njia ya Mwenye Enzi Mungu ikiwa wewe mwenyewe utaliridhia litokee, halazimishwi mtu katika hilo.
Sasa Jee Ushakutana na Rafiki wa Peponi?
Jee huyo unayeishi naye unataraji uwe naye  pamoja peponi, usifurahi ukaona kama nakupa ufunguo sasa ingieni, laa panataka kazi,(Isiwe kama Hadith ya wale mke na mume walopendana wakataka kuishi pamoja peponi, siku walogombana mwanamme kalala akaota kaingia peponi kakaa kwenye kiti wanapita Mahrul-ein, mara akahisi mtu anampiga kwenye bega ikisha akamnongoneza nipo, yule bwana kugeuka anamuona Mkewe kikamtoka kibao usingizini)msiwe kama hivyo hamtoipata pepo abadan, mtamalizikia na maradhi na majonzi maisha yote, sasa vipi mnatakiwa kukaa wewe na mwenzio, Hapa itabidi tujikumbushe maneno ya Kipenzi wetu Mtume s.a.w aliposema "Atakapo (funga)Ndoa Mja, itakua kakamilisha Nusu ya Dini, na huko Kumcha Mungu (Taqwa)ni nusu ilobakia" umepita katika Robo ya kwanza ya mtafutano, sasa umeingia katika nusu na jambo la kuoa au kukutana na mwenzio Bwana Mtume s.a.w kalihusisha na Nusu nzima ya Dini,(Nini Dini?)Dini ni mwenendo mzima wa Maisha, na hili la ndoa inakua ushafika nusu njia, ndio maana ukizini inakua umetenda Dhanbi kubwa, umerejea kwenye Robo, umefanya ufisadi, umetoka kwenye njia, wewe umedhulumu, ushapewa nusu nzima bado unatafuta na nusu za watu, ndio ikaamrishwa mpige makwaju mia huyu hafai kabisa, tena na zaidi mtangazie kwa jamii huyu mzinifu, huyu anayachafua maisha, huyu hatosheki, Mua anao ndani anakwenda kuokota Maganda yake, wakati Mua huo huo anaweza kufanya (Juice)au kutengeneza Sukari, mwenzenu huyu mgonjwa.
Jee ushakutana na Rafiki yako wa Peponi? Pata habari hii ili upate kujirekebisha, upate kurejesha mapenzi, upate kuridhika na ulichonacho. Imekua Nusu, sababu kutokana na hayo mapenzi nyinyi mekutana, kutokana na hayo mapenzi Mollah kakupeni watoto, akakutieni huruma kuvilea vitoto hivyo kwa uangalifu na unyenyekevu mkubwa, akakuleteeni furaha katika maisha yenu mkawa na afya mnacheka na kulia pamoja, vitoto vinakua vikubwa huku mkiviona, akawa Mollah wenu anakuruzukuni pasi hesabu, kwa njia za kila aina mnapata mstakbali wenu, vipi leo wewe unakua katili kwa (Your Other half)vipi leo unamuendea kinyume mwenzio, vipi leo unafika kumpiga na kumtolea ukali mwenzio, kwanini humpi heshima anayokupa wewe, kwanini huiweki nyumba yako ya Ardhini salama na Amani ili na ya huko Akhera iwe yenye mfano huo huo kama utaingia.Jitahidi sana uwe mbora na mzuri wa Roho kuliko mzuri wa sura na Mwili.
Vipi utajua umekutana na mwenzio, kuna mifano mingi ya kukujulisha huyu kweli ni mwenzangu, kwanza kabisa tizama tabia, vipi mnavyopendana, Mahusiano ya Kiroho daima yanakua si yenye masharti lazima uwe tajiri au uwe na cheo, au uwe mzuri, vipi maisha yenu yanavokwenda, jee Baraka zinatushukia baina yetu, isiwe ukatizama Baraka za riziki tu bali hata afya, furaha vinapatikana kwa mwenzangu huyu, Na kama kuna machafuko itumie nafasi hii kuanza kutafakari sasa vipi utabadilisha na kuituliza hali hiyo, la Mwanzo kabisa fanya uwe karibu sana na mwenzio huyu, achana na Marafiki wa Kidunia, itafute siri hii yakua huyu nilonaye hivi sasa pia tutakua pamoja tukiondoka kwenye Ulimwengu huu, Jaribu kuwa mstahamilivu, fanya upole kama mwenzio mkali, kuwa mtiifu kwa mwenzio na kumfurahisha kila ukipata nafasi, Muhimize bila ya kuchoka mkamatane katika njia ya Ibada kwa ajili ya Mwenye enzi Mungu, Jaribu kupata ukaribu wa kushikana mikono, kaeni pamoja katika mazungumzo, peleka ishara za mapenzi usisubiri mpaka uwe na matamanio ndio uanze kumkurubia mwenzio, ukifanya hivyo utajua kama kweli umekutana na mwenzio au unaishi na mtu anayekudanganya. Na ukiligundua hilo kunakitu kitatokea ambacho kitakujulisha ama kweli huyu mwenzangu, nini kitu hicho?. Endelea Part 3


No comments:

Post a Comment