Asalaam Aleiykum,
Sasa inakuaje mimi na wewe Tunateseka? Tunateseka Sababu hatumtegemei Mwenye-enzi-Mungu, na yanokutesa ni haya ya kujipa Ushujaa, unakua mwenye kutaka zaidi, unajinasibu kwa kipato chako, Unashughulika na Maisha uloyachagua wewe ya kutafuta Mali, na zaidi kujitegemea kwa maarifa yako. Unatafuta utajiri kwa njia yoyote, Akili yako hata ukenda Nyumbani bado inabakia katika mbinu za kujitajirisha zaidi, Na kama utakua Maskini ndio mama yangu, balaa tupu, Baina ya wawili nyie hapana tafauti yoyote, nyote hamumkumbuki Mwenye enzi Mungu, mkikutana msikitini, maskini anangoja kuomba na Tajiri anasubiri kuombwa, Kila mmoja ana fikra zake vipi atamkaba mwenzie, vipi atakumbukwa Mollah katika mazingira kama hayo, na Mwenye enzi Mungu anaendelea kukumbusheni katika Quraan Adh-Dhaariyat 55:"وَذَكِّرۡ فَإِنَّ ٱلذِّكۡرَىٰ تَنفَعُ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ"
Na Endelea kuwakumbusha, maana ukumbusho huwafaa wanoamini.
Umo katika kukumbushwa nguzo hii muhimu ya (Qadir)unatakiwa kama Muumin wa kweli uanze kutafakari, yasome maisha yako, jirudie wewe mwenyewe ujikumbushe kuna mambo mangapi yamekutokezea kwa ajili ya Inshaa Allah, wacha kioo sasa kamata kalamu hebu yaandike, inaweza kuwa cheo, au mkeo au mumeo jinsi mlivokutana, inaweza kuwa mali ulivoipata, wewe una dalili nyingi za Inshaa Allah zimefanya kazi katika maisha yako lakini huzikumbuki, hebu zirejee ili zipate kukurudisha katika Imani.
56"وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ"
Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu.
Unachotakiwa ni Ibadah, ikisha mengine mwachie yeye Mollah wako atakuongoza kwa njia usozifahamu, tena bila ya dhiki wala misukosuko, kwa sababu mwenye kukuongoza ndio anajua kakupangia nini.
58"إِنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلرَّزَّاقُ ذُو ٱلۡقُوَّةِ ٱلۡمَتِينُ"
Hakika Mwenye enzi Mungu ndiye mtoaji wa riziki, Mwenye nguvu, (Na aliye)Madhubuti,
Naam hivyo ndivo ilivyo Imani, huku ndiko kuishi kwa kutegemea Inshaa Allah, hayo ndio maisha ya Kiroho ya kuamini mimi nimeumbwa na yupo Mwenye kunipa Riziki yangu, Lakini ukiishi kwa Kutegemea Akili yako, unayakaribisha mateso, baada ya kichwani mwako kumjaza Mwenye enzi Mungu, zinajaa Biashara, kinajaa Cheo, na Baada ya hapo Akili limefurika, vipi Utapunguza ili upumzike, unatafuta (Kosha Roho)lazima upate kitu cha (Siri)pembeni, na hakuna jengine ila upate(Kimada).
Maisha ya Inshaa Allah ndio Mollah wetu anayotaka sisi tuishi ikiwa tunamuamini kweli, katupa(Challenge)anatutaka tuabudu tu, ikisha mengine tumuachie Yeye, lakini wapi, hilo ndio lenye kutushinda, tunaacha kuabudu ikisha hao tunakwenda kutumia Masaa 15 kazini, na huku zinakushinda hata dakika 5 za kuabudu, Na kila ukitumia muda wako katika kutafuta haya unayoyaona mafanikio, na huku unazidi kwenda mbali na Mollah wako, Unazidi kuikimbia (Laa Ilah illah Allah)usije ukadhani mbona sitoki Msikitini, mbona nasimamisha Sala zote 5, sikatai kweli unayafanya hayo, lakini hebu katika hizo Sala zako jichunguze Unamsabahi Mollah wako, au unaendelea na mambo ya ofisini, au unapanga faida za biashara, au unaamua kesi ya watoto,pengine unatatua jawabu la mtihani, tizama nini kimo katika hiyo Sala, halafu ndio utajua mimi niko karibu na Mollah wangu, au karibu na mambo yangu.
Usije ukasema huyu anosema haya yeye yukoje, mimi niko kawaida hata (Kanzu)sivai, wala ndevu sina, usinifate ukaniuliza mbona hututishi, sina haja ya kukutisha, ninachofanya kukupa (Ukweli)ukiona unafaa chukua utie moyoni mwako, huna haja ya mwengine kujua anza leo Kuishi Mwenyewe kwa kutegemea Inshaa Allah, huna haja ya kumhadithia mtu isije Inshaa Allah ikakutoka, Na maisha haya yana Mtihani sio Rahisi ukaona si nikubali tu, ukiamua kuingia katika Maisha haya jijue sasa wewe umeamua kujiunga na Waumini, unajiunga kuwa Mcha Mungu, na ukitaka kujiunga lazima kwanza utizamwe jee huyu mkweli, jee kweli unaitegemea nguzo hii madhubuti ya (Qadar)ya Mwenye enzi Mungu, Basi kama kweli umejizatiti sawasawa wacha nikupeleke chumba cha Mtihani. Endelea Part 4
No comments:
Post a Comment