Sunday, June 2, 2013

MARAFIKI WA PEPONI PART 3

Asalaam Aleiykum,

Kinatokea kitu kipya baada ya Umri wenu kusogea, na kama kweli mumeishi kwa wema na uaminifu, kusameheana na kupendana kikweli, hapo mapenzi yanapotea hadharani na kubakia moyoni kama vile mwanzo nilivo hadithia, hadharani inabaki Rehema ya Urafiki wa Kiroho unaodumu milele kwa kusaidiana na kuwa pamoja kwa hali na mali, unabaki umoja ulofunganisha (familia nzima kuwa kitu kimoja).Yanapotea matamanio na kubaki Maradhiano ya Kiroho katika mambo ya Ibada na Taqwa, kila mmoja anakua mbioni kujitaarisha na safari ndefu ya kwenda kukutana na Mollah wake na kutaraji kufufuliwa na kupewa Zawadi ya Mapenzi ya kukutanishwa na mwenzie tena na kuingizwa Peponi kuishi humo Milele kwa mapenzi na Furaha.
Na Mwenye enzi Mungu anatupa ahadi kwa wale alowapa zawadi hii ya kuwakutanisha katika Ulimwengu ikisha wakafanya nini?
Quraan sura ya Muumin aya ya 8,
"وَٱلَّذِينَ هُمۡ لِأَمَـٰنَـٰتِهِمۡ وَعَهۡدِهِمۡ رَٲعُونَ"
"Na ambao amana zao na ahadi zao wanaziangalia"
Mwenye enzi Mungu anakupa amana kadhaa ikiwemo hii ya kufunga (Ndoa)yakua umekutana na mwenzio na sasa unaamua kuishi maisha ya sheria za Kiroho, na unachukua ahadi yakua utaingalia amana hii na nyengine atakazo kukabidhi Mollah wako kama watoto na kadhalika, sasa ole wao wale wenye kuwanyanyasa  wanawake au wanaume, hao wamevunja kile kiapo cha ahadi, na yatakayo wafika basi wajue wameyataka wenyewe hakuna wa kumlaumu.
Na ikiwa umeishi kwa uangalifu katika Ulimwengu huu, ukatenda wema na kujiepusha na mabaya basi Mollah wako anakuahidi katika sura ya Zukhruf aya ya 68 mpaka 71
"يَـٰعِبَادِ لَا خَوۡفٌ عَلَيۡكُمُ ٱلۡيَوۡمَ وَلَآ أَنتُمۡ تَحۡزَنُونَ"
"Enyi waja (wangu wema)hamtakua na hofu siku hiyo wala hamtohuzunika"
Nyinyi mlikua mkitenda mazuri katika dunia, mkiishi uzuri na wenzenu, mkiwafanyia ihsani, mkistahamiliana,mkipendana,mkitizamana kwa macho ya huruma ikisha kubwa zaidi ni hili:
"ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ بِـَٔايَـٰتِنَا وَڪَانُواْ مُسۡلِمِينَ "
"Ambao waliziamini aya zetu na walikuwa waislamu kamili"
Kumbuka maneno ya Bwana Mtume s.a.w "Nusu ilobaki ni" "Kumcha Mollah" Na huo ndio Uislamu kamili ulokusudiwa hapo, kwanza umeziamini aya, halafu ukakamilisha hayo maisha(Dini) na kuwa Mkamilifu, nini sasa malipo yako kutoka kwa Mollah wako.
"ٱدۡخُلُواْ ٱلۡجَنَّةَ أَنتُمۡ وَأَزۡوَٲجُكُمۡ تُحۡبَرُونَ"
Ingieni Bustanini(Peponi)nyinyi na wake zenu(na humo)Mtafurahishwa.
Sasa kutana na Mkeo, kutana na Rafiki yako uloishi naye kwa wema, mkawa mnapendana na kumtii Mollah wenu, ingieni pamoja mkaone Raha za huko peponi.

"يُطَافُ عَلَيۡہِم بِصِحَافٍ۬ مِّن ذَهَبٍ۬ وَأَكۡوَابٍ۬‌ۖ وَفِيهَا مَا تَشۡتَهِيهِ ٱلۡأَنفُسُ وَتَلَذُّ ٱلۡأَعۡيُنُ‌ۖ وَأَنتُمۡ فِيهَا خَـٰلِدُونَ"
(Humo)Watakua wanapitishiwa sahani za Dhahabu na Vikombe, Na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.
Naam yote hayo mtayapata, wanakuhudumieni wafanyakazi wa Mbinguni, mtapata humo huo utajiri mnaoumezea mate hapa Duniani, na jua kila unachokipenda nafsi ikakosa katika Ulimwengu huu basi utakikuta huko kesho uendako, kama unapenda ugali wa muhogo utaukuta kwa magunia, na yale yote macho ambayo yalikua yanafurahia na hurusiwi pengine kuona huko utawekewa wazi ili upate kuviona, kwa hiyo usisikitike sana kama unavikosa hapa Ulimwenguni jua utavipata vyote kwa idhini ya Mollah wako.
Ila hapa duniani zidisha subira, jifunze kukinai, wacha tamaa na kaa vizuri na mwenzio ili upate kufanikiwa kwa hayo mazuri ya Peponi ambayo tunamuomba Mollah wetu aturuzuku kwa Uwezo wake.Amin.

No comments:

Post a Comment