Sunday, June 16, 2013

MAISHA YA INSHAA ALLAH PART 4

Asalaam Aleiykum,

Sasa ingia Chumba cha Mtihani uone kama kweli utapasi, fungua sura ya Baqarah aya ya 155 ili upate kuyajua maswali ya mtihani huo. 
"وَلَنَبۡلُوَنَّكُم بِشَىۡءٍ۬ مِّنَ ٱلۡخَوۡفِ وَٱلۡجُوعِ وَنَقۡصٍ۬ مِّنَ ٱلۡأَمۡوَٲلِ وَٱلۡأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٲتِ‌ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ"
"Na tutakutieni katika Msukosuko wa hofu na njaa na upungufu wa Mali, wa watu na matunda, Na wabashirie(Wafahamishe)habari njema (wale)wanosubiri"
Naam limetumika neno moja la tutakutieni, ili upate kuzinduka, ikiwa kweli unataka kufaulu mtihani huu basi mwanzo kabisa ingia ndani ya hofu ishi ndani ya hofu, ichambue hiyo hofu kumbuka usije kupigana nayo, hofu daima inashinda na hofu ikishinda hapo balaa ndipo inapoanzia, kwanini ikaanzia hapo, sababu mwanaadamu ni Kiumbe pekee mwenye kutaka zaidi. Mollah wetu katupangia jambo moja ana hakikisha hili la Mahitajio ya lazima analikamisha pasi na wasiwasi, Lakini mwanaadamu ni mwenye kutaka lake la zaidi na hapo ndio hofu inakaa kiti cha mbele na kukutoa kwenye Inshaa Allah na kukuongoza kwenye Uharibifu.
Lau ungejua hofu ni kama Kivuli, basi usinge idekeza, na ukawa unaipalilia, hofu ndio inakupeleka utake cha kuweka Akiba, hapo ndipo safari ya Maradhi yote ya vita vya Maisha inapoanza, hapo ndio (Round About)ya kumsahau Mollah wako, kama utakua Maskini unataka utajiri, na kama Tajiri unataka  Mali izidi(na aya imekwambia inapunguzwa)Na ukichunguza utagundua vita vyote vya Upuuzi, wewe na tajiri nyote mnakula chakula cha aina moja, pengine tajiri atakuzidi kwa (Ladha)yeye kautia nazi, au wake wapilau, lakini chakula ni kilekile, Shibe ni ileile,usingizi ni uleule, pumzi ni zilezile, sauti ni zenu ni hizo hizo, mwendo wenu nyote wa miguu miwili, kuona kwenu kote ni kumoja, akiumwa na wewe unaumwa, akikasirika na wewe unakasirika, katika Shani hii ya Mahitaji Mollah kaweka usawa, ila tafauti yenu mmoja kaamua kuishi Maisha ya Inshaa Allah na huyu wa pili kaamua kutumia mbinu zake, Na wewe ukiwa na mbinu zako, na wengine wanazao.
Vinaanza vita hapo kila mmoja kashatoka katika Njia ya Inshaa Allah hakamatiki, sasa unakua umeitafuta njia yako mwenyewe, tizama sasa ukiingia katika vichochoro hivi vya njia yako mwenyewe unakuaje, unakua una hofu, giza nene sijui itakuaje, unaendelea kupata dhiki mja wewe, kama una duka ukenda kusali unalibeba kichwani, sijui wanaiba, sijui nitapata faida, kama uko ofisini sasa unaogopa huyu mtoto mdogo aloletwa atachukua nafasi yangu au vipi, jee huyu ana haja na hichi cheo, unasahau hata kama Mungu alikuweka hapo mwanzo, na huyo unakimbilia kwa (mzee mlilo-jina la kubuni)eti akulindie cheo, na yeye anakutia mtihani anataka kitambaa cheusi ulookota barabarani, sijui mnaambiwa mlete na kucha za simba, eti ulindiwe mali au cheo hasara gani zimetufika hii leo, kawa mganga ndio mwenye kuilinda riziki, Shetani katutoa katika Maisha ya Inshaa Allah(Majaaliwa), katupeleka kwenye (Manyago)matupu, kichupa kiweke kwenye (Mafile)chukua Pete hili usilivue, wewe wakati unasoma ukapata hicho cheo mganga alikua wapi, basi hutumii hiyo akili hata kidogo.
Na ukiingia katika maasi hayo jua matatizo makubwa yanafatia, unaanza kuteseka, utaona mtu ana mali lakini hafurahi na mali yake sababu ya maradhi matupu, au kutwa anatafuta mali akirudi nyumbani usiku kucha anafunga hesabu hapati hata neema ya usingizi, na ukikosa usingizi unakuja wasiwasi ndipo unatafuta watu sasa ufatane nao, huna raha kabisa.
Na Maskini na yeye baada ya kumtegemea Mollah wake kwa Inshaa Allah, Laa na yeye anatoka mbio kwenda kupigana na maisha, na yeye anataka utajiri, anapotea kichochoroni na kumsahau Mollah wake, unamuona Msikitini lakini mawazo yote yapo kwenye doti za kanga alokopa atazilipa vipi, deni la fulani atamkwepaje, na vipi ataimaliza nyumba yake, hivo ndio sote maisha tunayoyachagua.
Sasa wenye kuishi Maisha ya Inshaa Allah wanakuaje?
Wnaishi kwa makubaliano na Mwenye enzi Mungu, wao wanakua ukinipa kula yangu, Alhamdulillah, ukininyima Laa Illah Illah Allah, Ukinipa cha zaidi Shukurani, ukininyima najua ndio kheri yangu, Mimi kwa upande wangu iajaribu, Najua na wewe Mollah wangu utanisaidia, mimi niwe muangalifu na mwenye subira, najua utanionesha ishara zako, zikiwa za kheri nizifate, na ikiwa za shari niziepuke, ukinipa kingi najua ni mtihani utokao kwako na ukininyima ni mtihani ambao mimi nimeukubali, Na kwanini nisiukubali hali ya kua wewe ndie uliyeniumba, ukanilea na kuninusuru nilivokua mdogo, nilipofikia wakati wa kufahamu Mollah wangu ukaniteremshia hekima ima niwe mfanya biashara au msomi, Na sasa naishi kama unavonitaka niishi kwa kukutegemea wewe Mollah wangu, na Maisha yangu yote nimekukabidhi wewe Mollah wangu muumba, nikiwa sina shaka utanitimizia kila mahitaji yangu yote. Na nitakapo taka cha ziada najua nimeamua kujitesa kwa jambo hilo.
Nakuomba Mollah wangu tujaalie Maisha haya ya Inshaa Allah tuwe wenye kukubali na kuiamini (Qadar)yako. tupe sisi Mioyo ya kufahamu kwamba wewe ndie mwenye kumpa huyu awe Raisi huyu awe Mfalme, yule awe Tajiri  na huyu aishi maisha ya kawaida, tupe sisi zawadi Adhimu ya kukumbuka kuwa wewe ndie ulotuumba na wewe ndie mwenye maamuzi yote ya Mustakbal wa maisha yetu. Na jengine la zaidi tupunguzie harakati za maisha zinazotupelekea mpaka tukakusahu wewe, halafu tupe utulivu wa Kiroho na Moyo ili tuweke nafasi ndani ya nyoyo zetu nafasi ya kukumbuka wewe wakati wote tukiwa macho na fahamu zetu, Kwani hiyo ndio Ibadah, huo ndio Ucha Mungu, na hayo ndio Maisha ya Inshaa Allah.

No comments:

Post a Comment