Sunday, May 25, 2014

MWANZO WA FURAHA KURIDHIKA PART 3

Asalaam Aleiykum

Na kaa ukijua Hakim wa haki analijua hilo na huwapa furaha kwa njia za maajabu wale walodhulumiwa. Sasa kwanini hatujaridhika?, Sababu kubwa hatuna Furaha, kwani lazima uwe na Furaha kwanza halafu ndio uridhike, kwanini ikawa hivyo hiyo ndio (Nature) kawaida ya maumbile, (Tizama wewe ukiwa mzima hupiti ukasema mie mzima, huna haja hiyo, lakini subiri ushikwe kidogo tu unavo tanganza naumwa mie, taabani ndio nakufa, unajua kwanini unasema hivyo kwa sababu furaha imeshaondoka, huridhiki tena mpaka upone).
Naam basi kwa kutaka ufahamu zaidi hekima ya Furaha na kuridhika tuhudhurie kisa hiki cha Mtoto na Baba yake kilosimuliwa na waja wenye hekima, "Baada ya kupita miaka mingi mtoto aliamua kurejea kwenda kuwasalimia wazee wake Kijijini kwao alipozaliwa, Ilipofika Magharibi wakakaa na Baba yake na kama kawaida Mzee akaanza kumuuliza Mwanawe vipi huko Mjini kuna Raha gani?, Mnatunyima nini watu wa mjini, Yule Mtoto akajibu ahh huko kuna vitu vya kila aina, Litizame swali la Mzee limeanza na nini? na Mtoto pia kaanza na nini? Mzee kaanza na Raha, na Mtoto kaanza na vitu, kumbuka vitu vinakaa nje, lakini Raha zinakaa ndani kwenye Jinsi yako.
Na hiyo ndio dasturi yetu viumbe sote, ila wachache tu waloigundua Raha wanajua haikai kwenye kitu, tuna tabia ya kuangalia kitu sana na ukiangalia kitu ina maana hujaridhika kwa sababu kitu hakileti Furaha, "Yule Mtoto akaendelea kusema Mjini kuna mataa na kuna meremeta sana kwa mataa hayo, Mjini kuna Magari mengi, Kuna Masenema, Kuna Mapesa, Kuna Watu, Kuna Mabiashara, Jee Baba Shamba kuna nini?.
Baba akajibu Mwanangu hapa kuna Raha, Kitu cha Mwanzo nasikia Furaha kuamshwa Kusali Alfajiri kwa Sauti ya kiumbe mwenzangu Jogoo, Nikimaliza Kusali Nasoma Quraan, Nikimaliza natulia kusikiliza Sauti za Ndege wanavo wasiliana kwa sauti zao nzuri, Ikisha Nakunywa Chai halafu huyo nashika njia kuelekea (Kondeni)Shamba huku nikimsabahi Mollah wangu, Ninapofika Shambani Nalima kwa Unyenyekevu huku nikimuomba Mollah wangu anipe alichonikadiria huku nikikumbuka maneno yaliyomo aya ya 7 sura ya (Talaq)
لِيُنفِقۡ ذُو سَعَةٍ۬ مِّن سَعَتِهِۦ‌ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيۡهِ رِزۡقُهُ ۥ فَلۡيُنفِقۡ مِمَّآ ءَاتَٮٰهُ ٱللَّهُ‌ۚ لَا يُكَلِّفُ ٱللَّهُ نَفۡسًا إِلَّا مَآ ءَاتَٮٰهَا‌ۚ سَيَجۡعَلُ ٱللَّهُ بَعۡدَ عُسۡرٍ۬ يُسۡرً۬ا 
Mwenye wasaa agharimu kadiri ya wasaa wake, Na yule ambaye amepungukiwa na Riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenye enzi Mungu, Mwenye enzi Mungu hamkalifishi Mtu yoyote ila kwa kadiri ya alichompa, Atajaalia Mwenye enzi Mungu baada ya Dhiki Faraji.
"Ewe Mwanangu zingatia sana maneno yaliyomo kwenye aya hiyo ukiyagundua maana yake utaingia ili uwemo kwenye Furaha" Baada ya kutoridhika utapata furaha, Ikisha huyo narudi nyumbani nikiwa na Furaha kumkuta Mke wangu keshapika, tunakaa wenyewe tunakula halafu tunapumzika, ikisha tena nyakati kama hizi za Usiku hapa hakuna Taa ila kuna Nuru ya Mwenye enzi Mungu ya Mbaa mwezi na Nyota ndiyo inayotumurika, baada ya hapo tunakwenda kulala salama usalimini hatuna fikra wala mawazo yoyote yanotupa wasiwasi au mashaka, Na wala hatukosi Rehma za Mollah wetu za usingizi.
Ila Mwanangu kuna kitu kimoja nataka kukujulisha ukifika usiku huja Simba akanguruma sana lakini usiogope, Hao wazee wakaaga kwenda kulala na yule Mtoto akaingia chumbani kwake lakini maskini hakuridhika kabisa akakaa macho anamsubiri Simba asikie Mngurumo wake, Na huku kashika panga labda simba atavunja Mlango, kitu cha ajabu chumba cha pili anasikia wazee wake wamelala wanakoroma, Na ndivo ilivo mpaka hivi sasa sote tupo tunasubiri Simba, Kila Mtu hajaridhika, kila mtu hana furaha, kila mtu hapati usingizi, na mifano tunaiona Mtu anajenga Jumba kubwa la Fahari ikisha analitia vyuma kwa kuogopa Simba, Na kama bado hajaridhika anaweka na walinzi, na ikiwa haijamridhisha anatia (Alarm) yote hayo yanafanywa kumsubiri Simba.
Na tumo hatujaridhika mpaka tusikie Ngurumo yake, Na kila tukipatacho haturidhiki, ukiwa Karani unautaka Umeneja, Ukiwa Mzuri huridhiki mpaka ujipambe zaidi, Ukiwa Tajiri huridhiki lazima uzidishe utajiri wako, ukiwa maskini ndio mama wee vita si vidogo, takriban maisha yetu yote tunoishi haturidhiki na wewe fanya uchunguzi uone umeridhika lini, na ikiwa hujaridhika basi huna Furaha, na kama huna Furaha unakosa jambo muhimu sana katika maisha haya, Na Mwisho nakukumbusha Ridhika na ukiridhika tu pale pale unaingia Furahani, na Furaha ndio maisha yenyewe usikae ukawa unaishi ndani ya Dhiki huku Faraja inakupita.


No comments:

Post a Comment