Sunday, August 31, 2014

MAISHA YA AKHERA PART 3

Asalaam Aleiykum

Sasa ikiwa ulohudhuria umepata bahati ya ukumbusho moja kwa moja unapata bahati ya kujua kwenye moyo wako sio katika Akili yako kuwa wewe sio hichi kiwiliwili wanachokizika, na ukiweza kumtizama huyo Maiti kama umepata huo ukumbusho utaona kuna kitu kimeondoka, kuna kitu kimepungua ukiligundua hilo (Eureka) hutokua kama zamani tena, utabadilika milele, utakua umegundua kitu ambacho watu wengi hawakigundui mpaka mwisho wa umri wao, kwanza itakuingia khofu ikisha yataingia mapenzi ya kutaka kujua zaidi vipi Maisha ya Akhera yakoje, pia utagundua kumbe katika Ulimwengu huu mimi ni mgeni, utagundua tafauti yako na kiwiliwili chako, utagundua katika Ulimwengu huu mimi sina Uhusiano wa kudumu na yoyote, mimi ni mpita njia ambaye naishi kwenye Ulimwengu huu kwa muda mchache sana, Ikiwa kiwiliwili kinafukiwa na wale walo wangu niloishi nao Ulimwenguni, Sasa hebu nifanye kujijua mie nani na safari yangu nakwenda wapi kuanzia leo, leo napata nafasi ya kujijua kuwa asilimia kubwa ya kiwiliwili changu ni hii Ardhi, ambayo hivi sasa wako mbioni kunirejesha kama ilivyosemwa kwenye sura ya (Taha aya ya 55)
 مِنۡہَا خَلَقۡنَـٰكُمۡ وَفِيہَا نُعِيدُكُمۡ وَمِنۡہَا نُخۡرِجُكُمۡ تَارَةً أُخۡرَىٰ 
Katika hii (Ardhi)Tumekuumbeni, Na Humo tutakurudisheni, Na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine (Tena)
Kuwa na hakika kwa mujibu wa aya hiyo kwamba utarejea tena katika maisha kama haya lakini kwenye mji wa Akhera, utapata kuelewa kumbe kinachokufa na kuzikwa ni kiwiliwili changu tu, lakini mimi mwenyewe niko hai na nashuhudia kufa kwa kiwiliwili changu na naendelea kusihi na Mauti hayanigusi ila na hama kwenye Ulimwengu huu na kuhamia huko Akhera ambako safari yake inaanzia Makaburini nilikoambiwa nikahudhurie, Huko Akhera, Jee kukoje huko Akhera, mie nitaishi vipi huko Akhera, nani atakua Mwenyeji wangu, mapokezi yangu yatakua vipi, hawa nilowaita wenzangu Ulimwenguni wananifukia na kunisahau jee Maisha yangu ya Akhera yatakua vipi.
Hayo ndio Maswala unayotakiwa kujiuliza, khasa ukijua Umri wenyewe ushakatika na ni muda mchache unaishi katika Ulimwengu huu, Mwaka wa hamsini huu wale wote walokwenda hawajarudi, wana hali gani huko Akhera, wanaishi vipi huko katika Mamlaka ya Akhera, namie nifanye nini nikenda huko niipate salama Usalimini, najua hapa Duniani nimepokewa na viumbe wenzangu nikakaa nao, wako walonichukia wakanidhulumu, wakanipiga, wakanipa machungu, nilogombana nao nikatenda nilotenda, ikisha nikachukua zawadi nzuri na mbaya sasa nini yatakua mapokezi yangu kwa hao viumbe nisowajua katika Maisha ya Akhera. Mollah nijaalie Radhi zako huko ninapokuja niwe nimefaulu, nisiwe katika Ulimwengu huu nimepata misukosuko na huko Akhera napata misukosuko, wapi yatakua makaazi yangu huko Akhera?

No comments:

Post a Comment