Asalaam Aleiykum.
Umeweza kurekebisha tabia yako ndani ya moyo mpaka ukapata Rehma ya Mollah wako inayoonekana nje, sasa hata ukiona vyakula japo unatamani huvigusi ila kwa wakati mahsusi tena kwa ajili ya Imani ya Mollah wako(Kwanini usisamehewe)hilo pekee ni Ishara nyengine. Kutokana na hali hiyo umeonesha una uwezo hata mengine unaweza kuyaacha ukitaka, ndio maana nikakwambia kwa ishara hiyo fanya ujute kwa makosa yalopita Mollah wako atakusamehe.
Na pia kumbuka huu msimamo ulo shika katika mwezi huu waweza kukusaidia hata baada ya Ramadhani kupita kwanini uweze mwezi huu na ushindwe miezi mengine jee umewahi kujiuliza swali hili, Nataka uelewe tabia za maasi ni adui wako basi kwanini huchagui tabia za kheri zenye malipo ya kudumu zenye kukuunganisha na Mollah wako, Basi hebu jitahidi ikisha Ramadhani ubakie na hizi tabia njema ulozimudu hivi sasa.
Kwa kukumbuka hayo tokwa na machozi kumbe unaweza kukaa bila ya kutenda makosa lakini umetawaliwa na kusudi, kwa kumuhofia alokuumba acha machozi yakumiminike na ikisha uweke ahadi katika kumi hili yakua "Ewe Mollah wangu ukinisamehe"sitorejea tena haya makosa ya kusudi, Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani Mollah kakupa nguvu kuweza kuyashinda mambo yote ya Shetani na vishawishi vyake na wewe angalau kwa siku hizi chache umepata daraja la Uwalii, Basi muombe Mollah wako asikuondoshee Rehma hii ili uwe umetubu toba ya moja kwa moja, kumbuka tafauti yako na walii yeye anadumu katika hali hii ya mwezi wa Ramadhani na wewe ni mwenye kupita njia, Basi ukitaka na wewe udumu katika ishara za kusamehewa hebu pata huzuni katika mwezi huu kwanini unashindwa kuendelea na tabia hii njema ya kufanya Taqwa.
Ukipata hisia hizo ujue Mollah wako kesha kukubali na wakati wowote anaweza kukushushia Rehma zake ukadumu katia hali hiyo.Sasa pata ishara zaidi za kusamehewa ukiwa nazo hata moja basi jijue umeingia katika kumi hili na umo katika Rehma ya (Toba).
Na Ishara zenyewe utakazozipata mja za kusamehewa, hebu utizame ulimi wako jee umebadilika, Unahifadhika wewe kwa mambo ya kusema uongo, kusengenya na uzushi pamoja na ufedhuli wa maneno, jee unaushughulisha ulimi wako kwa kusoma Qur'aan na kumkumbuka Mollah wako.
Ishara nyengine ya kusamehewa jee unajichunga na sheria za tumbo kuwa huli isipokua cha halali.
Ishara ya kusamehewa jee unaikumbuka Amri ya macho hutizami mambo ya haramu na wala huangalii matamanio ya kidunia yakaku sahaulisha Mollah wako, isipokua macho hayo yawe yenye kudumu kutizama ufalme wa Mollah wako na mafunzo yake.
Na Ishara ya kusikia inayokufanya usamehewe, Amri za sikio kusikiliza mambo ya maasi ikawa kutwa umedumu katika kusikiliza mipasho ya uongo,habari za watu, kusengenya nk. Jitizame wewe nini yanaingia masikioni mwako, jee sauti za kheri zilojaa makumbusho ya Mollah wako zinapita katika shikio hilo.
Na ishara inayofatia ujijue umesamehewa, jee unajiepusha na maamrisho ya mikono wewe, hukamati au kubeba vilivyo haramu, au kuchukua mali isiyokua halali yako,Na kama vile kukishika kile usojuzu kukikamata, mfano kumshika mwanamke asokua muharim wako,(kama kupeana mikono).Basi inatakiwa mikono hiyo idumu kufanya amali za utiifu kwa ajili ya Mollah wako.
Na ishara inayokujulisha kusamehewa kwako ni kama hii miguu, jee huendi wewe kwenye sehemu za maasi na uchafu, ila uwe unakwenda katika misikiti na kufanya kheri za jihad na sehemu za mambo ya kheri.
Na ishara zengine za kusamehewa zilochupa katika moyo, basi usafishe moyo wako kwa uadui katika dunia hii, usafishe na uhasidi kwa ajili ya watu(ondosha husda)ujaze moyo wako mambo mema na maombezi kwa wenzio na uwe mtu wa nasaha kwa wenzako.
Na japo zipo nyingi hii ya mwisho ya kufungia maudhui yetu ishara yake ya kusamehewa ni kuhusu Ucha Mungu wako uwe mwenye Ikhlas kwa ajili ya Mwenye-enzi-Mungu, Ujiepushe na mambo ya (Riyah)kiburi na jeuri kwa wanaadamu wenzako.
Basi mwenye kuzipata ishara hizi japo moja na hali yakua yumo ndani ya kumi la maghfira basi ajijue yumo katika kundi la kusamehewa na (Inshaallah Mwenye-enzi-Mungu atujaalie tuwemo katika walokubaliwa msamaha)Amin.
A.Baja
No comments:
Post a Comment