Saturday, July 27, 2013

WAJUE WALOFUNGA MWAKA HUU PART 1

Asalaam Aleiykum,

Tunaingia katika kumi la kuchukuliwa (Dhamana) na Mollah wetu, Dhamana hiyo ni kuepushwa na adhabu za kila aina, zikiwemo za kaburi, adhabu za maisha na ile adhabu kubwa iumizayo ya Moto wa Jahannam siku hiyoo ya Malipo, Lakini jee dhamana hii anaipata kila mtu? Jawabu utalipata ukizama katika darsa hii ili kujijua unastahiki hiyo dhamana, Jee umo katika fungu la walofunga? au unasubiri mshituko gani utaupata ikiwa hesabu zako zote zitaishia katika fungu la walokaa na njaa. Nini habari ya waliokaa na njaa? nakuchukua wewe msomaji ili ufikirie hali gani utakua nayo kama utaalikwa shughuli, upo hapa duniani fulani kakualika shughuli na wewe umehudhuria, Ikisha likatoka tangazo wenye kula biriani wasubiri kwanza, sababu unatolewa wali mweupe, halafu baada ya wali mweupe kumalizika, anatangaza mtangazaji walokula na wasokula nyote ahsanteni kwa kuhudhuria, Jitizame vipi utakua kisa kama hicho kikikutokea na wewe una njaa, na nyakati saa nane za mchana, jua linawaka kwa vishindo, vipi itakua hali yako? hali kama hiyo ndio itatokea siku ya Kiyama pale watapoitwa wale wote walokua wakifunga wapite mlango huu wa Rayyan, na wewe kwa vile unajiamini umefunga unafata, mara unasikia umekamatwa ngozi na (Malaika)unarejeshwa nyuma rudi, huku unadhani mie nilikua nafunga vipi leo mambo haya? ukisema mimi nilikua sili wala sinywi, unajibiwa hiyo ilikua sio saumu, wewe ulikua ukifanya(Diet).
Nani Walofunga?
Walofunga ni wale ambao walikua wakifanya (Taqwa)ipasavyo, Na yoyote yule alofanya Taqwa ikatimia kikweli hana haja ya kujijua, ukiona unaanza kujiuliza jee mimi nimefanya Taqwa basi jitilie wasiwasi, na ufanye haraka kufata muongozo wa darsa hii huko mwishoni ili uipate hiyo Taqwa. Mwenye kufunga kweli hana haja ya kujua kakubaliwa au kakataliwa, yeye huyo anakua kazama katika hisia za Taqwa na ana fahamu alitendalo kama anavofahamu hili jua, huu mwezi, na huu mchana, hana haja ya yeye kuambiwa huu mchana, sasa hivi wewe umacho, ukiwa macho moja kwa moja unajijua mimi ni macho, na kama hivo ndio anavojijua mtenda Taqwa, lakini alo lala usingizi yeye ndio hajui nini kimetokea, yeye yupo wapi, na kufunga ndio nini, sasa ikiwa umelala usione uchungu tutakuamsha upate kufunga japo hizo siku kumi za mwisho ili na wewe uipate (Swaum).
Nini Taqwa?
Maana ya Taqwa ni Mapenzi, na mapenzi ni khofu ya kuogopa usimkere Mollah wako aliyekuita katika Mwezi huu Mtukufu wa kumtii yeye ambao ni huu Ramadhan,  Sasa jihadhari ikiwa umo katika lile kundi liloshindwa kwanza kabisa kuzuia Macho na mambo yote ya Haramu, (basi wewe utakua miongoni wa wale wenye kutaka kuwajua walofunga) Huna Taqwa, ila una njaa.
Na kama bado unapinga yakua Swaum unayo basi hebu jiulize umempa Mollah wako heshima kwa ajili yake ukajizuia na kujiepusha na maovu haya ya macho. Na katika huko kuona kuna namna mbili ile ya bahati mbaya Mollah wako anaijua, nini habari yako wewe ulofanya kwa kusudi? jee (Umo katika kundi la walofunga)majibu tambua mwenyewe. Wewe bado umebakia katika mwezi wa kula mchana, hujaingia kabisa katika Mwezi huu wa Ramadhan, Ama yule aliyekuwemo kwenye Ramadhan yeye anakua kashaigundua (Switch) na kama huijui hii (Switch) basi wacha nikujulishe ili na wewe upate kuitumia siku za mbele, na kama utaweza kuitumia nyenzo hii itakusaidia sana katika matendo yako ya Kuona, Wewe una (Switch) mbili lakini kwa muda huu huzielewi ziko wapi na zinatumika vipi, kuna hali mbili zinakutokea na ukitaka kuyajua hayo sasa endelea part 2

WAJUE WALOFUNGA MWAKA HUU PART 2

Asalaam Aleiykum,

Hali ya mwanzo jaalia hivi umepinda kichochoro, ukakutana na mti mzuri, angalia nini kinatokea ndani ya mwili wako(Nothing happen)katika hisia zako, halafu nenda mbele zaidi ukutane na mwanamke au mwanamme mzuri, sasa angalia tena hali gani unakua ndani ya kiwiliwili chako, Sasa kama utakua mwerevu basi ushazigundua (Switch)mbili basi itumie (switch)iloona mti, kwani hii inapatikana kirahisi mwezi huu wa Ramadhan, ndio maana ukaambiwa (kufunga)kunakata matamanio, itumie (switch) hii mwezi huu na miezi mengine ukiwacha kuangalia matamanio utawasha (Switch) ya Taqwa, ambayo ndio inayotakiwa katika mwezi huu ili upate kufanya shughuli za Taqwa kwa utulivu, inawezekana pia kutumika (Switch) hiyo  katika kusikia, kwani tayari unaitumia lakini hujui matumizi yake kwa njia ya ufundi muda huu. Sasa wacha nikufahamishe vipi inakua (Switch) ya kusikia na kazi zake, tuseme una sikiliza Quraan, unasikia jogoo linawika, gari inapita, ndege wanaimba, lakini yote hayo yanapita sikio hili na kutokea upande wa pili, na masikio yako yamelenga kwenye Quraan pekee unaisikiliza na kuifahamu, na yale mengine umeyasikia lakini hayaja kushughulisha kabisa, na hivo ndivyo inavotakiwa katika mwezi huu uwe mwenye kusikiliza mambo mema, umo katika mwezi huu tumepita katika macho na masikio ili turejee katika Taqwa ya Ramadhan, na sisi tuwemo katika walofunga, usikate tamaa, bado unao wakati wa kuiwahi gari ya mwisho isije ikakuacha, irekebishe Swaum yako uwemo katika kundi la walofunga. Nani alofunga? alofunga wakati wote anajijua yeye yumo ndani ya Swaum, inakua hajajizuia na kula na kunywa tu, bali alofunga  kazuia kauli zake hapiti akitukana ovyo na kutoa maneno machafu, hendi kila pahala na kusengenya watu, ndani ya kifua chake marfuku katika mwezi huu mzima kutoa kauli nzito nzito za kujeruhi wenzie na kuwashtumu kwa jambo hili na lile, umo kutaka kumjua alofunga basi mtizame yule asonyanyua mkono na kumdhuru mwenzie, wala kuchukua kisicho halali yake, mwiko kwake kumdhulumu mtu, na Wala hanyanyui miguu yake kwenda kokote anako asiwa mpenzi  Mollah wake, aliyeipata Swaum hajishughulishi na kauli chafu, hatoi ukali wala kugombana, hafanyi mambo ya kipuuzi wakati huu wa Taqwa, hamkejeli mtu na kujiona yeye bora, daima hukumbuka mimi nimefunga, kila akiona maovu hukumbuka mimi nimefunga, akiona mambo ya kipuuzi anakumbuka mimi nimefunga.
Alopata Swaum anakua kafunga masikio, kafunga macho, kafunga ulimi, kafunga mikono, kafunga miguu baada ya hayo yote kuyakamilisha, sasa anafungua mlango wa Taqwa. Ukoje Mlango huo endelea Part 3

WAJUE WALOFUNGA MWAKA HUU PART 3

Asalaam Aleiykum,

Watu wengi inapofika katika kufanya Taqwa wanakua hawajui nini hasa msingi wa Taqwa, Mti huu wa Taqwa una matawi mengi madogo madogo, kama vile kutoa sadaka, kuhurumia wazee na wagonjwa, kutoa zaka na  matawi mengi mengine, lakini inapofika katika mti wenyewe watu wanaganda hawajui wafanye nini, mtu hana mashiko wala dalili, haelewi vipi afanye aipate hiyo zawadi kubwa ya mapenzi ya Allah, vipi atakutana na kile kisicho onekana, afanye nini atosheleze nafsi yake ili ajue ama kweli mimi nimepata (Contact) na (Beyond), Sasa leo mtaniwia Radhi ili nikuchukueni kwenye hii safari japo nusu njia ili nikuoneshe vipi utapata hiyo Taqwa ya Mwenye enzi Mungu, ambayo katika mwezi huu ni kusudio lenyewe, igundue siri ya wanofunga na kufanya Taqwa wanakua katika hali gani kwenye mwezi huu ili na wewe ujiunge nao.
Nipeni ruhusa nizungumze sura ya Al-Imran aya ya 190 mpaka 191, ili tupate kugundua hiyo Taqwa ikoje na vipi ukurubie kwa Mollah 
wako,
 "إِنَّ فِى خَلۡقِ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ وَٱخۡتِلَـٰفِ ٱلَّيۡلِ وَٱلنَّہَارِ لَأَيَـٰتٍ۬ لِّأُوْلِى ٱلۡأَلۡبَـٰبِ"
"Katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutafautiana (baina)ya usiku na Mchana, kuna alama (Ya kuwapo Mwenye enzi Mungu) kwa wenye Akili".
kwanini ikatajwa Mbingu kuumbwa kwake na wewe hujaishuhudia, sababu katika Mbingu ziko alama, na sasa mnasomeshwa, ukizitizama mwenyewe nyota unaona zinakwenda, kuna nyota zile tano zinoonesha pembe zote za Ulimwengu huu, kuna mambo ya kila aina huko juu, lakini mchana hatuyaoni tumefunikwa na hii taa ingarayo kwa mwanga mkali, na katika hii ardhi, ukiwa mcha Mungu wa kweli utaona mambo ya ajabu ya kila aina, kuna alama kwa Mabilioni zimetuzunguka, lakini wengi hatutumii akili hata wakati huu wa Swaum ambapo akili imetulia na inaweza kugundua mambo mengi, hebu angalia vipi maisha yalivo, tizama wanyama kila mtu alivopangiwa shughuli zake, Ndege ana mambo yake, vidudu vina mambo yao, paka ana mambo yake, mpaka kuku ana shughuli zake za pekee, na wanaadamu hali kadhalika kila mmoja ana fikra zake na matendo yake, ikisha kuyaona hayo, halafu tizama sote tulivo pewa uhai, sote tukawa tunaishi kwa amri yake Ikiwa Mcha Mungu au umepata Swaum kikweli basi utaangusha macho chini ikisha useme kwa hilo Mollah wangu nathibitisha kuwepo kwako pasipo na shaka yoyote, na pia nasadikisha hili halipati yoyote yule alojaza kichwani mwake mambo  chungu nzima ya kidunia katika mwezi  Mtukufu wa Ramadhan.

"ٱلَّذِينَ يَذۡكُرُونَ ٱللَّهَ قِيَـٰمً۬ا وَقُعُودً۬ا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمۡ وَيَتَفَڪَّرُونَ فِى خَلۡقِ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ رَبَّنَا مَا خَلَقۡتَ هَـٰذَا بَـٰطِلاً۬ سُبۡحَـٰنَكَ فَقِنَا عَذَابَ ٱلنَّارِ "
"Ambao humkumbuka Mwenye enzi Mungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala, Na hutafakari umbo la mbingu na ardhi,(Na wakasema)Mollah wetu hukuviumba hivi bure, Utukufu ni wako, basi tuepushe na adhabu ya moto"
Linapotajwa neno kukumbuka watu wengi wanadhani ni ile (dhikr) walizozisikia za kwenye (Mazawiya na zinazofanyika mashamba) hapo kukumbuka sio kusudio hilo, kusudio la hapo ni kukumbuka kwa Mcha Mungu, na wewe umo kwenye mwezi wa Ramadhan unafanya Taqwa, basi ipate maana ya kukumbuka huko, ili hizo siku kumi zilobaki uwemo katika kundi la walofunga, Kukumbuka kuliko kusudiwa hapa ni kule kila saa na dakika, hususan kwenye mwezi huu wa Ramadhan, hebu pata maana ya neno Muabudu Mollah wako kama unamuona, lina maanisha uwe unajua popote ulipo uwe unafahamu Mollah wako pia ni mwenye kukuona, chochote ukifanyacho uwe unatambua Mollah wako ni mwenye kushuhudia,Ukikaa kitako ukamuona kipepeo anaruka,  uwe unaziona alama za Mollah wako, vitoto vinacheza ukumbuke na wewe uliwahi kuwa kama wao na sasa Mollah wako kakufanya umekuwa mkubwa kwa malezi yake,Mshipa wa swaum ukikushika ukataka kulala usikumbuke maandazi na machopo chopo, ila mkumbuke Mollah ana kujulisha mshipa wa Swaum na kukuangalia mja wake, ukikaa na wenzio wao wanacheka wewe mkumbuke Mollah wako useme,Mollah wangu nikurubishe kwenye Ufalme wako , unifanye kuwa kipenzi chako, Usininyime mimi ladha ya hata dakika moja kuto kukumbuka wewe Mollah wangu,nipe mie uwezo wa kukumbuka nikiwa kazini, nikiwa barazani, nikiwa popote pale ambako waja wako wamekusahau, basi naomba hii hadhi ya Ucha Mungu initeremkie niwe na sifa ya kukumbuka, na pia uwe unatambua Mollah wako anazungumza na wewe kwa lugha mnayofahamiana, mfano kama vile anavo kunusuru na mabalaa na unajua kuna kitu ndani ya hisia zako kimekwambia leo usende pahala fulani, au unasema Roho yangu nzito, halafu unasikia ahh imetokea ajali watu wamejeruhiwa vibaya sana, baada ya kugundua umezungumza na Mollah wako, unazuka na kusema (Machale yamekucheza) au ukinusuriwa na dhuluma au kuibiwa unasema umecheza kama Pele, unaonesha jinsi gani ulivomsahau Mollah wako. Ila unamkumbuka wakati mmoja tu unapotaka kuomba au ukiwa unaumwa, hapo dua na Sala zitatumwa na machozi, lakini nyakati zote humjui kabisa na yanakutoka hata kama umeumbwa.
Basi husema wale wenye kuishika Taqwa na kuipata Swaum, Ya Raab hakika hukuumba haya bure tu ndio iwe basi, Hakika umetukuka Mollah wetu basi na sisi tumo kwenye Swaum, na Hili linaloingia ni kumi la dhamana ya kuepushwa na Moto, basi na sisi tunakuomba utunusuru na Moto wa Jahannam.
Endelea part 4

WAJUE WALOFUNGA MWAKA HUU PART 4

Asalaam Aleiykum,
Ikiwa umo kwenye Swaum na umeipata kweli kweli basi moyo wako lazima uwe maridhia kwa hukumu na amri zote za Mwenye enzi Mungu, aliyefunga mwezi huu anajishughulisha sana na kusoma Quraan, Sasa wacha tukugeukie wewe tukutizame na hiyo Swaum yako, umefanya mangapi katika hayo, jee umewahi kuipata hata saa moja katika mwezi huu kuitumia kwa ajili ya kumfikiri Mollah wako na alivyoviumba, umeufanya mwezi huu ni kwa ajili ya kutafuta mapenzi ya Mollah wako, kumbuka yeye ndie aliyekuumba na hivi karibuni utakwenda kukutana nae, basi ikiwa hujafanya hivyo basi kumbuka umebakisha siku kumi za mwisho, acha kila kitu upate kuwahi ili na wewe uwemo katika walofunga, mkimbie mwenye kukuita kwenye karata, sasa ni kipindi cha kuacha kutuma msg kwenye wassup.acha katika kumi hili kusikiliza muziki na kutizama Tv, utumie muda huu kumkumbuka Mollah wako kwa wingi, ipate Itikaf uisikilize salamu zinazokuja kwenye moyo wako, punguza kuuza na kununua ili uzijue kheri za Ramadhan, kakae uzidishe ibada asaa yaweza kuwa mwaka wako wakuipata Lailatul Qadir, tegemea aya  ya 35 Fussilat inavosema

" وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ٱلَّذِينَ صَبَرُواْ وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ۬ "
Lakini (Jambo hili)hawatapewa ila wanosubiri, (Na)wala hawatopewa ila wenye Bahati kubwa(hadhi mbele ya Mollah wao)
hii inaweza kuwa usiku wako, hakikisha haukupiti hata mmoja katika hayo masiku kumi, Mkumbuke Mollah wako usiku akukumbuke mchana, mkumbuke kwenye furaha atakukumbuka kwenye shida, mkumbuke kwenye Swaum ili akuingize kwenye Pepo ya Al-Rayyan, Zidisha Ibada zako daima uwe Furahani. Mollah zipokee Ibada zetu, utusamehe Dhanmbi zetu, turidhie matendo yetu yawe kwako yenye kukuridhisha. Tunakuomba Neema na kheri zako zitushukie katika mwezi huu.Amin.


Saturday, July 20, 2013

MAOMBI YA TOBA(KUMI LA KUSAMEHEWA)PART 1

Asalaam Aleiykum,

Mollah wetu ametuumba wanaadamu ikisha akatufanya si wenye kuepuka vitendo vya Dhanmbi, akatutenganisha viumbe sisi kuwa tafauti na Malaika, ikisha tena akatuwekea njia ya Mitihani katika mambo mawili, la kwanza  ni Amali za kheri na la pili zile amali za shari, Ikisha akamfahamisha tena jambo la tatu nalo hili la kufanya Taqwa,  kwa ajili ya kumtizama kama kweli kiumbe changu kina mapenzi na mimi Mollah wake Muumba, Na jambo  la nne akamjulisha hiyo shughuli ya matamanio huku akiwa anamjua udhaifu wa kiumbe chake, kutokana na kufahamu vyema udhaifu huo ndio akamuekea hili la tano nalo ni  zawadi ya kumsamehe.
Jambo hili la Msamaha leo ndio tunaingia katika kumi lake, hii ni sehemu maalumu ilotengwa kwa wale watotaka kuomba msamaha, Sasa kwanini Mwezi huu na hususan ndani ya kumi hili?.
Sababu kubwa mwezi huu ikiwa kweli umefunga kwa dhati na Imani ilothibitika wa hiyo (Taqwa) basi ni lazima kumi la mwanzo lilopita ushapata hiyo Rehma, kwa Maana hiyo umesha safishika na sasa uko tayari kurejea kwa Mollah wako(Usishtuke sio kufa maana yake hilo mnaogopa sana)kurejea hapo ni kusudio la hiyo (Toba) Tayari sasa mapenzi yashakuvaa katika mambo ya kidini, tayari ushaanza kuonea huruma viumbe wenzako, Na sasa umeingia katika (Stage) ya kuitakasa Roho yako kwa kuomba (Maghfira)Msamaha kwa Mollah wako.
Msamaha wenyewe kwa yale yote ulotenda dhidi ya Mollah wako na pia kwa Viumbe wenzako, Hivi sasa wewe Umeshagundua kuwa Dhanmbi zimekuzunguka kila upande, yaweza kuwa dhanmbi za Husda au Chuki, umezifanya za Ufisadi au zile za Uhasama, Umetenda dhanmbi za wivu na zile za Macho na Masikio, kuna zile ulizo zisahau, na hizo unazozikumbuka. kuna zile za Ulimi na hata hizo za Mawazo machafu au mabaya zote hizo zinatakiwa ziombewe Samahani, Na ukijitia Ujabari huombi Msamaha siku ya Hukumu utafungwa nazo shingoni huku unapelekwa kuhudhuria mbele ya Enzi ya Mollah wako.
Kwanini Usitubu? Wakati Bwana Mtume s.a.w anasema katika hadith(Sharif)"Enyi Watu Tubuni kwa Mollah wenu, hakika mimi mwenyewe kwa siku natubu mara mia moja". Inawezekana wewe Mpaka leo ya kumi hujatubu hata mara tano, sasa leo umeingia hili kumi la (Maghfira)Kusamehewa, basi kama hujaanza, basi anza leo kutubu na kama umeshaanza basi zidisha idadi na mara zako za kutubu ili uwe mwenye kufanikiwa, Ewe mja anguka kwa Mollah wako utoke chozi, halafu ujute kwa yote uliyoyatenda, na wala usione unayefanya ni wewe bali hata mitume wa Mwenye-Enzi-Mungu na wao wamefanya makosa na wakatubu, na kama unataka ushahidi wa hayo na vipi kupata maneno ya Toba endelea Part 2

MAOMBI YA TOBA (KUMI LA KUSAMEHEWA)PART 2

Asalaam Aleiykum,

Nini Kutubu? Kutubu ni kukumbuka kuwa yupo aliyeniumba, namie kwa heshima zote narejea na kugaragara chini ya Enzi yake ya kusamehe, nikitaraji yale yote nilotenda Mollah wangu atanisamehe, Na mimi nimo kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhan, katika mwezi huu nimo katika kukumbuka, basi wacha nijiunge na wale walotajwa katika sura ya Al-Imran 135

وَٱلَّذِينَ إِذَا فَعَلُواْ فَـٰحِشَةً أَوۡ ظَلَمُوٓاْ أَنفُسَہُمۡ ذَكَرُواْ ٱللَّهَ فَٱسۡتَغۡفَرُواْ لِذُنُوبِهِمۡ وَمَن يَغۡفِرُ ٱلذُّنُوبَ إِلَّا ٱللَّهُ وَلَمۡ يُصِرُّواْ عَلَىٰ مَا فَعَلُواْ وَهُمۡ يَعۡلَمُونَ
Na ambao wanapofanya Uchafu, au kudhulumu nafsi zao, hukumbuka Mwenye Enzi Mungu na kuomba Msamaha kwa Dhanmbi zao, Na Nani anayeghufiria dhanmbi isipokua Mwenye Enzi Mungu, Na(Wala)hawaendelei na (Mijidhanmbi)waliyoyafanya, hali wanajua.
Wametajwa kwenye hiyo aya wale wanofanya Uchafu, kwa kumaanisha dunia hii ni safi, njia imenyooka, ila wewe ndie unaekuja na visa na mikasa, ukauchafua Ulimwengu huu kwa dhanmbi chungu nzima, na kila ukiona watu wanasafisha kila ukichafua, basi hapo tena  unarejea nakuanza  kudhulumu nafsi yako mwenyewe kwa mambo chungu nzima yalokuzunguka, lakini ukitanabahi na kujua yupo aloniumba mimi na anastahiki kuabudiwa na kuombwa Msamaha, basi hakuna mwengine atakaye kusamehe isipokua yeye Mollah wako, kama walivosamehewa wengine walopita kabla yako.
Basi wakumbushe kisa cha Nabii Daud a.s pale alipompenda Mwanamke akaamua kumpeleka mume wa Mke huyo ambaye aliyekua Jeneral wake vitani, huku akijua fika hatorejea yuko hai, jikumbushe nini kilitokea, Quraan sura ya Sad aya ya 21-25
" وَهَلۡ أَتَٮٰكَ نَبَؤُاْ ٱلۡخَصۡمِ إِذۡ تَسَوَّرُواْ ٱلۡمِحۡرَابَ"
Na jee imekufikia habari ya wagonvi walipopindukia(Ukutani)chumbani(Kwa Nabii Daud). Nabii Daud alikua na jeshi lenye nguvu na ulinzi Mkali, walipoingia (Hawa Malaika wawili)ilikuaje.
"إِذۡ دَخَلُواْ عَلَىٰ دَاوُ ۥدَ فَفَزِعَ مِنۡہُمۡ‌ۖ قَالُواْ لَا تَخَفۡ‌ۖ خَصۡمَانِ بَغَىٰ بَعۡضُنَا عَلَىٰ بَعۡضٍ۬ فَٱحۡكُم بَيۡنَنَا بِٱلۡحَقِّ وَلَا تُشۡطِطۡ وَٱهۡدِنَآ إِلَىٰ سَوَآءِ ٱلصِّرَٲطِ"
Walipomuingilia Daud na (yeye)akawaogopa, Wakasema Usiogope, (sie ni )wagombanao wawili, Mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe, basi (sasa)tuhukumu,(toa uamuzi baina yetu)Kwa haki wala usipendelee, na utuongoe katika njia iliyo sawa.
Na nyinyi pia wenye madaraka, viongozi, wenye uwezo, mawakili mnajiwa na watu na kesi kama hizi, wanakujieni maofisini na majumbani watu kudai haki zao ili , Muhukumu kwa njia ya haki, tena wanakwambieni nisaidieni mimi nimedhulumiwa nini unamjibu, Huna jawabu ila kula Rushwa, huna Jawabu ila kuchangia dhuluma, huna jawabu ila kuleta fisadi ndani ya mji.
"إِنَّ هَـٰذَآ أَخِى لَهُ ۥ تِسۡعٌ۬ وَتِسۡعُونَ نَعۡجَةً۬ وَلِىَ نَعۡجَةٌ۬ وَٲحِدَةٌ۬ فَقَالَ أَكۡفِلۡنِيہَا وَعَزَّنِى فِى ٱلۡخِطَابِ"
Hakika huyu ni ndugu yangu, yeye ana kondoo majike tisini na tisa, na mimi nina kondoo mmoja tu jike,lakini amesema, nipe huyu wako nikufugie,  Na amenishinda katika maneno.
Na nyinyi hali kadhalika  anakuja mtu pengine ana viwanja 99 lakini kakipenda kile kimoja hakiwezi kukikosa, basi hapo unamtilia Mawakili na vitisho hivi na vile, mpaka mnamshinda maskini yule kwa maneno ikisha hao mnakichukua kiwanja au kitu chengine mlofanikiwa kukipata kwa njia ya wizi.Tena mnaruhusu wengine ndugu kudhulumiana, kwa kuwa ana uwezo na kashakupa chai.

" قَالَ لَقَدۡ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعۡجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِۦ‌ۖ وَإِنَّ كَثِيرً۬ا مِّنَ ٱلۡخُلَطَآءِ لَيَبۡغِى بَعۡضُہُمۡ عَلَىٰ بَعۡضٍ إِلَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ وَقَلِيلٌ۬ مَّا هُمۡ‌ۗ وَظَنَّ دَاوُ ۥدُ أَنَّمَا فَتَنَّـٰهُ فَٱسۡتَغۡفَرَ رَبَّهُ ۥ وَخَرَّ رَاكِعً۬ا وَأَنَابَ "
Akasema kweli amekudhulumu kwa kukuomba kondoo wako kuongeza katika kondoo wake, Na bila shaka washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipokua wale waloamini na kutenda mema, na hao ni wachache:Na mara Daud akaona kwamba tumemtia mtihanini(Na amefeli)Akaomba maghfira kwa Mollah wake, na akaanguka (Kwa)Kunyenyekea na Akaelekea kwa (Mollah wake).
Haijambo huyu Mtume wa Mwenye Enzi Mungu, kapata ukumbusho na kuzinduka, Na wewe pia unapata ukumbusho kama huo ila tafauti yake wewe unaendelea na vitimbi vyako, na hivi ndivo ilivo dhihiri mambo ya dhuluma, kila mtu katoka kwenye dini yake, kila mtu anataka mali, hakuna huruma, watu wamesahau hata kuomba msamaha ni kitu gani, hiyo ni habari ya dhuluma na kutubia kwa Mtume wa Mwenye enzi Mungu, na kuna kisa cha Musa a.s yeye alivompiga mtu ngumi akamuua akamuomba Mollah wake amsamehe sura ya Qasas aya ya 16"
"قَالَ رَبِّ إِنِّى ظَلَمۡتُ نَفۡسِى فَٱغۡفِرۡ لِى فَغَفَرَ لَهُ ۥۤ‌ۚ إِنَّهُ ۥ هُوَ ٱلۡغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ "
Akasema Mollah wangu, bila shaka nimedhulumu nafsi yangu, basi (Naomba)nisamehe, Naye (Mollah)akamsamehe, (Sababu hakufanya kwa kusudi) hakika yeye ni mwingi wa kusamehe (na)kurehemu. hilo pia tendo la Mauaji, na kama utarudi kikweli kwa Mollah wako basi utamkuta  yeye mwenye kukusamehe.
Sasa endelea part 3 ukapate hayo maneno yakuombea toba na ujue yalianzia wapi.

MAOMBI YA TOBA(kUMI LA KUSAMEHEWA)PART 3

Asalaam Aleiykum,

Napenda ufahamu vitendo vyote ulotenda vipo vimeandikwa na wala havifutiki mpaka viombewe msamaha ili upate kuepukana na adhabu ya siku ya Kiyama, Inabidi lazima ufunge safari ya kutubu ili upate kuepuka kuangamia siku hiyo ya hukumu, Sasa hii kutubu imeanzia wapi, kapewa nani? na je wewe pia unapewa maneno haya na muongozo huu, Kihudhurie kisa cha Nabii Adam a.s alipo kosa na kuletewa maneno ya kutubu.
"فَتَلَقَّىٰٓ ءَادَمُ مِن رَّبِّهِۦ كَلِمَـٰتٍ۬ فَتَابَ عَلَيۡهِ‌ۚ إِنَّهُ ۥ هُوَ ٱلتَّوَّابُ ٱلرَّحِيمُ "
Akapokea Adam maneno(Ya Maombi)kwa Mollah wake(akaomba)na Mollah wake akapokea toba yake, hakika yeye ndiye mwingi wa kupokea toba, na mwingi wa kurehemu.
Ewe Ndugu yangu umo katika Mwezi wa Ramadhan, na katika aya hiyo yametajwa maneno mawili muhimu kutubu na rehema, ama kumi la mwanzo ni kumi la kurehemewa na hili kumi la pili ndilo la kusamehewa, na wewe unafanya nini? Mwenye enzi Mungu kakujaalia kila usiku unafanya kitu gani?, huu sio mwezi wa kukesha kwenye Tv, wala kwenye gumzo ila mwezi huu unatakiwa uwe unafanya nini? jawabu la kufanya utalipata sura ya Adh dhaariyat 17mpaka18"كَانُواْ قَلِيلاً۬ مِّنَ ٱلَّيۡلِ مَا يَہۡجَعُونَ  "Walikua wakilala kidogo(nyakati)za usiku" "وَبِٱلۡأَسۡحَارِ هُمۡ يَسۡتَغۡفِرُونَ"Na wakiomba Msamaha (Maghfira) Nyakati za kabla ya alfajiri" Na wewe si unahudhuria (Sala ya Taraweih) si Unasali (Qiyyam layla) basi umo katika hao, sasa midamu ushalipata kumi la rehma, basi na sasa pia una uwezo na wewe kupokea maneno ya Mollah wako ya kutubu, na sio lazima yaje kama alivopewa Nabii Adam a.s, lakini yanaweza kuja kwa njia nyingine na mifano mengine, kama ukumbusho huu ya kuwa leo ukumbuke dhanmbi zako zote za nyuma, na kuanzia leo uwe unalia kwenye msala na kujuta, na kudhamiria hutofanya tena, wewe unakiri umekosea  kwenda kushinda kwa waganga, kumdhulumu fulani, na kama yuhai nenda ukamlipe, kama yupo mbali mpigie simu, (hatopata kukupiga ngumi)umtake samahani,kama Umezini huu ndio wakati wa kutubu, kuna ulowatia maradhi kwa matendo yako, kuna ulowadhuru kwa maneno yako, kuna ulowahasidi kwa kuwasingizia mambo chungu nzima, sasa umepata nafasi katika kumi hili taka radhi za Mollah wako, Omba msamaha ili upate kusamehewa, na utakapomalizika mwezi huu endelea kutenda mema kwani kutenda mema kumetajwa katika sura ya Furqan aya ya 70.
"إِلَّا مَن تَابَ وَءَامَنَ وَعَمِلَ عَمَلاً۬ صَـٰلِحً۬ا فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ يُبَدِّلُ ٱللَّهُ سَيِّـَٔاتِهِمۡ حَسَنَـٰتٍ۬‌ۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورً۬ا رَّحِيمً۬ا"
Ila yule atakayetubia  na kuamini na kufanya vitendo vizuri, basi hao ndio Mwenye enzi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema, na Mwenye enzi Mungu ni mwingi wa kusamehe (na) mwingi wa kurehemu. yale yote ulofanya ya uovu yatabadilishwa kuwa mema ikiwa kweli utazidisha wema wako. Mwenye enzi Mungu anakupa hekima na muongozo na unakumbuka hili nifanyalo ni kosa, huu mwenendo si mzuri, hapo jijue unapewa (chance) ya kutubu, ili upate kuwacha na kurejea kwa Mollah wako, na unapopewa fikra hizo za kutambua hilo ni kosa basi chunguza nyuma ya fikra hizo kuna neno Msamaha, basi omba msamaha haraka, kwa yale ulotenda ujanani, miezi ilopita au ndani ya mwezi huu kwa kutizama yalo haramu na kula vya haramu, sasa uombe vipi ? hakuna atokufundisha maneno ya kusema ila yeye Mwenyewe Mollah wako, na kama hufahamu hayo maneno unayopewa Moyoni, basi angaku na ujitupe kwa Mollah wako kwa maneno haya ya Toba ili yakuanzishe safari yako ya Kutubu.
"Ewe Mollah wangu Mwenye kujua siri na dhahiri, Mimi nilikua najidanganya katika kukuasi wewe, na sasa niko katika enzi yako yenye kumiliki huu uhai, mimi nimegundua nilofanya hayastahiki kuniweka mimi karibu na wewe, lakini kwa ruhusa ya rehma yako ulonikatia mimi, nakuomba nianguke mbele ya Enzi ya uweza wako ulonijaalia mimi kuweza kukukmbuka, na nikiwa katika mwezi huu Mtukufu ulonitengea ili nifanye Taqwa kwa ajili yako, basi nakuomba kwa dhati ya moyo wangu, UNISAMEHE, natanguliza kwako ahadi ya kutofanya tena maovu nikiwa na Imani kwa hilo utanisaidia, Na nyenyekea katika Enzi yako ya kusubiri, ile ambayo ilikua  ikinisubiria  wakati wote nilokua nikikuasi, Nateremsha mimi hii akili na vilivyomo ndani ya mwili huu, pia naondosha jeuri na viburi vyote nilobeba kwenye mabega yangu, nakuja mimi nikiwa nimebeba mizigo ya Madhanmbi na kuangusha kichwa hichi kwa sijida nikitafuta radhi na msamaha utokao kwako Mollah wangu. Katika Ufalme wako Mollah wangu sina mimi jitihada wala ujuzi wa vipi kujua kama utanisamehe au hunisamehe, lakini nimebeba Imani yangu nikiamini mapenzi yako juu yangu ya huku kuniumba na mimi kukubali na kufanya Ibadah kwa ajili yako, hilo linanipa Imani ya kuamini Mollah wangu utanisamehe kwa Uweza wako."Ewe Mollah wangu hakika mimi nimezama katika kiza cheusi cha madhanmbi, nimekabiliwa mimi na shetani Ibilis katika kila nyanja ya maisha yangu, mpaka jambo la Sala Mollah wangu ananipoteza Shetani Muovu, basi Naomba kwa dhati ya uweza wako Nikinge mimi na Shetani ili nisirudie kukuasi tena katika maisha yangu, kwa Fadhila za Mwezi huu wa Ramadhan na mengine itofata, nakuomba Mollah wangu wasamehe Walo fariki na walo hai, wape uzima waja wako wote wenye maradhi, wape wepesi wale wote wenye dhiki ya maisha, waondolee matatizo kwa kila wenye kuwafika balaa, ututie sote Peponi kwa uwezo wako Yaa Subbhanna.Amin".

Sunday, July 14, 2013

MTIHANI WA TAQWA PART 1

Asalaam Aleiykum,

"Ewe" Muumin umo katika kumi la mwanzo, kumi la Rehma, Ndani ya kumi hili inakupasa tukupe peni na karatasi ikisha tukuingize katika chumba cha mtihani, Na chumba chenyewe ni huo Msikiti au hata Chumbani kwako unapofanya Ibadah, halafu ufanye nini ukisha kuingia, kaa kimya au kaa Itikaf upate kuikamata karatasi ya maswali uanze kulijibu moja baada ya jengine hayo yaliyomo kwenye hiyo karatasi.Maswali yenyewe ya huu mtihani yanahusiana na Taqwa, mwisho wa mtihani huu utajua Mwenyewe jee unafanya Taqwa au unaiga kufanya Taqwa. Majibu utakayopata kwa uyakinifu yatakupa nafasi katika mwezi huu wa Ramadhani ya kujirekebisha, au kama utataka kuendelea kama ulivyo, pia huo ni uamuzi wako, na wala hakuna atokulazimisha ukichagua kuwa (Muflis) katika mambo ya Dini.
Unafanyiwa Mtihani huu kutokana na aya moja tu katika sura ya Baqarah aya ya 177,

"لَّيۡسَ ٱلۡبِرَّ أَن تُوَلُّواْ وُجُوهَكُمۡ قِبَلَ ٱلۡمَشۡرِقِ وَٱلۡمَغۡرِبِ وَلَـٰكِنَّ ٱلۡبِرَّ مَنۡ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلۡيَوۡمِ ٱلۡأَخِرِ وَٱلۡمَلَـٰٓٮِٕڪَةِ وَٱلۡكِتَـٰبِ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ وَءَاتَى ٱلۡمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِۦ ذَوِى ٱلۡقُرۡبَىٰ وَٱلۡيَتَـٰمَىٰ وَٱلۡمَسَـٰكِينَ وَٱبۡنَ ٱلسَّبِيلِ وَٱلسَّآٮِٕلِينَ وَفِى ٱلرِّقَابِ وَأَقَامَ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَى ٱلزَّڪَوٰةَ وَٱلۡمُوفُونَ بِعَهۡدِهِمۡ إِذَا عَـٰهَدُواْ‌ۖ وَٱلصَّـٰبِرِينَ فِى ٱلۡبَأۡسَآءِ وَٱلضَّرَّآءِ وَحِينَ ٱلۡبَأۡسِ‌ۗ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ ٱلَّذِينَ صَدَقُواْ‌ۖ وَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡمُتَّقُونَ"
Sio wema(Taqwa) kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharib(Katika Kusali)Bali wema(Taqwa)ni (wale)wanomuamini Mwenye enzi Mungu na siku ya mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, Na wanawapa mali (Zile) wanozipenda, Jamaa (Wakaribu)na Mayatima na Maskini na Wasafiri(Waloharibikiwa njiani)na Waombao na katika (kuwakomboa) Watumwa, Na wakawa wanasimamisha Sala na Kutoa Zaka, Na watekelezao Ahadi zao wanazoahidi, na Wavumiliao katika shida na dhara wakati wa vita, hao ndio walosadikisha(Dini yao)Na hao ndio Wamchao Mungu(Wafanyao Taqwa).
Umo katika Ustaadh wa Kulea Roho wacha nikuchukue pole pole ili upate kujiangalia jee japo kwa uchache mimi ninayo japo matatu katika mambo hayo, Yanatakiwa matatu ili upate kufikiriwa labda unaipata hiyo Taqwa. basi kwa kuanza huo Mtihani endelea part 2.

MTIHANI WA TAQWA PART 2

Asalaam Aleiykum,

Angalia vizuri sana ikiwa Una Madaraka sehemu yoyote, au wewe mfanya Biashara, au una maisha ya kawaida kama mimi na wewe pamoja na umaskini wetu, utaona aya hii imetukusanya sote kama hupo juu basi chini imekuhusu, na wajibu wa aya hii ni kutukumbusha nini Taqwa, Imekusanya aya hii chanzo cha Mapenzi ya Imani, Kwanini nikataja Imani na nisitaje Kuamini, Kwa sababu kuamini ni rahisi sana(Beliving) Tizama mtoto siku zote anavokuamini unapo mdanganya nikirudi nitakuletea(Sweets)na ukirudi huleti, au unakwenda senema mpaka unatoka unaamini (mkubwa wa Adui)kafa kweli, hivyo ndio kuamini. Lakini (Trust) au Imani ni kitu chengine kabisa, na hicho hakihusiani kabisa na kuamini, Sasa hiyo Imani ikoje?, Imani ilokusudiwa katika hiyo aya ni hiyo (Trust) kabla ya kuendelea mbele zaidi wacha nikujulishe mifano miwili mitatu ya hiyo Imani au (Trust) inakuaje.
Imani inaishi ndani ya Kifua chako na hujitokeza japo kwa uhafifu pale ambapo , tuseme unapanda Ndege, Jiangalie wewe unakua hali gani, Huku Wahudumu wanakuhimiza ufunge mkanda, wanakwambia kama hukufunga hatari tupu, mpaka simu zimeni isije ikatufika balaa, au likatokea la kutokea, tena unazidishiwa habari kwa kuambiwa kama itatokea dharura yoyote au mambo yakizidi pumzi za (Oxygen) tutakupeni sisi, baada ya vitisho vyote hivyo hakuna hata mtu mmoja anaeomba kushuka, unajua kwanini, Sababu (Deep inside of you) kuna Imani (Trust), hapo tena ndege hiyo inaruka na huku dua zinakuporomoka, kwa mara ya mwanzo pengine inakujia walotengeneza ndege hii wamepata ujuzi wao kutoka kwa Mnyama ndege, na kutokana na Mnyama huyo Mwenye enzi Mungu kasema katika sura ya Mulk aya ya 19,

"أَوَلَمۡ يَرَوۡاْ إِلَى ٱلطَّيۡرِ فَوۡقَهُمۡ صَـٰٓفَّـٰتٍ۬ وَيَقۡبِضۡنَ‌ۚ مَا يُمۡسِكُهُنَّ إِلَّا ٱلرَّحۡمَـٰنُ‌ۚ إِنَّهُ ۥ بِكُلِّ شَىۡءِۭ بَصِيرٌ"
Jee hawaoni Ndege walioko  juu (Angani) wanavo zinyoosha (Mbawa zao)na kuzikunja, Hakuna anayewazuia (wasianguke) ila (Mwenye enzi Mungu),Mwingi wa Rehma, hakika yeye anaona kila kitu. Na mimi sasa naweka Imani yangu yote kwa Mollah wangu ili anivue salama dege hili lisije likaporomoka.
Na kadhalika mkiwa Baharini vilevile Bahari imechafuka nyote mnarejea kwa Mollah wenu na Ahadi na madua makubwa makubwa, Au Mtu akiumwa anakua na Imani mpaka pale anakata Roho, au ukenda kulala unakua na Imani Asubuhi utaamka, basi hizo kwa uchache ni dalili za kuijua hiyo Imani, ili huko mbele katika safari yetu itakapotajwa Imani ujue tunazungumza nini, na tumekusudia kitu gani, Hiyo ndio Imani iliyo tafauti na kuamini.
Sasa Wacha nikupeleke chumba cha mtihani, Na Mtihani ukianza nakuomba kitu kimoja kifanye kwa ajili ya manufaa yako, Utakapoona alama ya Kuuliza (?)na neno funga macho basi jifanyie Ihsani ya kweli yafunge macho yako ili jawabu liwe lako mwenyewe na sio unikopie, hasara yake ukikopia utabakia daima hujui, daima huchunguzi, daima unaamini na unakua huna Imani.
Endelea part 3

MTIHANI WA TAQWA PART 3

Asalaam Aleiykum,

Sio wema (Taqwa)kugeuza shingo zenu Mashariki wala Magharib katika kusali, tizama ikiwa Sala mwanzo imekataliwa haimo katika (taqwa)mpaka vipatikane viungo vyake, nini habari ya Saumu yako wewe na mimi, Nini wema(Taqwa) Ni Kumuamini Mwenye enzi Mungu, Jee wewe Unamuamini (1)? (Funga Macho kabla ya kuendelea utupe vigezo vyako) Mimi nitakupa kigezo kimoja na vyengine utatafuta mwenyewe. 
"Nakuamini Mollah wangu kwa kujijua mimi ni nani na nipo katika Ulimwengu huu kwa ajili gani, Nakuamini Mollah wangu pale ninapoangalia Ulimwengu huu na vyote viliyomo, hususan nikitizama  vinyama, awe mdogo au awe mkubwa halafu najitizama na mimi mwenyewe kwa huu Uhai ulotujaalia sote, yananitoka machozi pale ninapoona umetupa sote Fahamu ya daraja kwa jinsi ya uwezo wetu, naona mimi vipi kinyama cha kila aina kinapotafuta Riziki yake na kuweza kujitosheleza, ukawapa fahamu pia yakujitafutia pahala pa kuishi, Ikisha kwa Rehma zako ukavijaalia vyote ikiwemo na mimi hii Neema ya Usingizi kuweza kulala na kuamka, Nautizama mpaka Mti Mollah wangu, nao unakula na kunywa na kulala, na kwa hilo Mollah wangu nasema umetukuka kwa sifa zote zisizo upungufu na mimi sina cha kutanguliza mbele yako isipokua kusema Alhamdullillah.
Nini wema (Taqwa)Kuamini siku ya Mwisho(2) ?(Fumba macho) Kwa ajili ya kuona kwangu katika Ulimwengu huu kila kitu kiko kwa muda, hakuna cha kudumu, kama mimi nilivokuja na kuna siku nitaondoka kama wenzangu walotangulia, hilo limenifikisha kuyakubali maneno yako yaliyomo kwenye sura ya Al-Rahman aya ya 26 "كُلُّ مَنۡ عَلَيۡہَا فَانٍ۬" Kila kilichomo juu yake kitatoweka(Ardhini na Mbinguni), basi kutokana na maneno hayo na matendo yako ya ishara yalodhihiri nina Imani pia kuna mwisho wa haya yote.
Kuamini Malaika (3)? (Fumba macho) Wacha nikuchukue nikupeleke ili ukajue vipi au wapi viumbe hawa unaweza kuwaona au kuona ishara zao kuwa wapo, hayo yote yanategemea wema wako (Taqwa) yako ilivyo, ili kuweza kufungua pazia hilo, usisubiri mpaka siku ya kutoka Roho ukaanza kusema mbona naona mtu kanisimamia, mbona haondoki,  huyu nani kasimama,usisubiri kufunguliwa pazia, fungua mwenyewe kwa kuzidisha (Taqwa). Sasa kutana au iyone hiyo kazi ya hao Malaika wawili ili upate kuamini, unaambiwa katika sura ya Qaf aya ya 17"

"إِذۡ يَتَلَقَّى ٱلۡمُتَلَقِّيَانِ عَنِ ٱلۡيَمِينِ وَعَنِ ٱلشِّمَالِ قَعِيدٌ۬"
"Wanapopokea (Malaika)wapokeaji wawili, anayekaa kuliani na (anayekaa)Kushotoni"
Hao ndio wanoandika  dhanmbi zako au thawabu zako, vipi utawajua ili upate kuamini, hakuna njia nyengine ila ujitizame kama unatenda dhanmbi kwa kusudi, nasema kwa kusudi kwa sababu ya bahati mbaya hutoweza kujua, ikiwa unatenda kosa ukalijua hili kosa, basi tazama upande wako wa kushoto nini kinatokezea katika (Mind)yako angalia sana kuna kitu utagundua, na pia kama unafanya jambo zuri angalia upande wako wa kulia kwenye (Mind) yako nini kinatokezea na vipi unakhisi, ukianza kuyagundua yanotokezea kidogo kidogo utaanza kuamini kumbe dooh kuna viumbe vimeniganda na vinaandika kila jambo.
Kuamini Kitabu chake(4)?(fumba macho) Wengine wanapoambiwa kuamini kitabu basi mbio mbio wanachukua Quraan na kuanza kuibusu kisha wanaitia kwapani huku wanaendelea kama kawaida kutesa wenzao, kudhulumu wenzao, kusengenya wenzao, wanavunja kila sheria iliyomo katika hicho kitabu, Maana halisi ilokusudiwa ya kuamini kitabu ni kuwa na Imani na maneno na amri alokupangia katika maisha haya, kakupa maisha ikisha kakuletea muongozo, sura ya Baqarah aya ya 2"

"ذَٲلِكَ ٱلۡڪِتَـٰبُ لَا رَيۡبَ‌ۛ فِيهِ‌ۛ هُدً۬ى لِّلۡمُتَّقِينَ"
Hiki ni kitabu kisichokua na shaka ndani yake, ni uongozi kwa wamchao Mwenye enzi Mungu.
Maana ya kuamini kitabu ni kutii na kufata yaliyomo katika hayo maandiko, na hayo ndio maisha alokutakia Mollah wako, umepewa Uhai na ukapewa muongozo wa kuifata njia ilonyooka, lakini ukijifanya jeuri au mjuaji ukachupa na kuingia msituni, basi hapo inakua ushapotea, na msitu kama unavoujua una miti mingi, una wanyama wa kila aina, na inabidi sasa utafute njia yako mwenyewe ili uipate tena njia ilonyooka, sasa katika kutafuta hiyo njia, ndio na wewe inabidi uandike Kitabu chako, lazima uje na Ramani lako la kutoka huko msituni, unatoka huko Simba washakuparura Kitabu kishachanwa, hapo unaambiwa  katika sura ya Al Haaqqa aya ya 19"فَأَمَّا مَنۡ أُوتِىَ كِتَـٰبَهُ ۥ بِيَمِينِهِۦ فَيَقُولُ هَآؤُمُ ٱقۡرَءُواْ كِتَـٰبِيَهۡ "
"Basi ama yule atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa kuume(kulia) atasema haya someni daftari langu". Mtu wa kheri hana cha kuficha maisha yake yote yako wazi, kakopia kitabu alicholetewa na Mollah wake,huyo atakua maisha yake yote ya Raha, ikiwa unaficha ficha basi jitilie wasiwasi siku hiyo usije ukawa  kundi la wanopokea kwa mkono kushoto aya  ya 25"
Endelea part 4

MTIHANI WA TAQWA PART 4

Asalaam Aleiykum,

"وَأَمَّا مَنۡ أُوتِىَ كِتَـٰبَهُ ۥ بِشِمَالِهِۦ فَيَقُولُ يَـٰلَيۡتَنِى لَمۡ أُوتَ كِتَـٰبِيَهۡ"
Lakini atakayepewa daftari(Kitabu)lake katika mkono wake wa kushoto basi yeye atasema (Bora)Laiti nisingelipewa daftari langu.
Unaangalia Kitabu sifuri tupu, unaona leo nitakiona cha mtemakuni.
Kuamini Manabii wake(5)?(Fumba macho) Hujawahi kuwaona wala kuwasikia vipi utaamini, hapo unamrejea Mollah wako akupe huo muongozo wa kuwaamini na kuwakubali Manabii wake, kutokana na ishara na athari walizoziacha, kutokana na maneno waliyoyaleta, na habari zao unazosomewa, halafu jifanyie mtihani ndani ya nafsi yako, hivo kweli Mtume s.a.w angekuwepo leo ningemkubali, mbona likitajwa jina lake sihisi kitu, mbona damu hainichemki, jee angekuwepo Nabii Isa a.s (Jesus) akanambia mtu akikupiga kibao mgeuzie upande wa pili ningekubali, vipi ningekutana na Nabii Musa a.s akanambia pita katika bahari ningemfata, ukipata majawabu hayo utajua nini Imani yako kuhusu Manabii.
Sasa wacha tuingie katika Barafu ya Moyo, wacha tuguse tuone vipi watu wanavoichukia Dini, tizama wangapi watazima Computer, kuna watofikia mpaka kutukana, kwanini, sababu tunagusa yanayowashinda wengi kutekeleza nayo ni hiyoo Mali, hiyo ndio Fitna ya mtu kukubali kuikosa Taqwa lakini abakie na Mali.
Na Wanawapa Mali(6)?(Funga Macho) Jiulize unatoa wewe Mali yako, huo Mtihani mkubwa, na mwanzo unaambiwa ile unayoipenda ndio itoke mwanzo, Una nyumba tatu, ile Flat ya Upanga unamtafuta ndugu yako wa karibu, hii chukua wewe, una Nyumba Baharini Mangapwani unamtafuta jamaa yako wa karibu wewe huna kitu hii chukua wewe, una gari mbili wewe za nini, na hupandi zote itoe kwa jamaa zako wa karibu, una mkufu wako wa dhahabu mpelekee jamaa yako huu shika wewe, maskini hamna hata pesa ya futari nendeni kauzeni ili mpate chakula, huo ndio ucha Mungu, Jee wewe unafanya hayo, Una mapesa Bank yamelaliana nje kuna Mayatima wangapi unatoa kwa ajili yao, Unawapa wewe Maskini, Mtu kakufata kaharibikiwa hana tiketi ya kurudi nyumbani jee unampa, anakuomba nauli unamfonya halafu unajiita Mcha Mungu, na wale wanoomba ukawapuuza yote ni mitihani Mollah anakuletea, anatumwa Muombaji aje kwako kwa kusudi, na wewe jitizame sasa umepata wasiwasi, eti wewe ndio unakimbia usiombwe, Na katika kuwakomboa Watumwa, Na kumkomboa Mtumwa sio lazima awe kanunuliwa, yumo umemuajiri mfanyakazi wa nyumbani, unamtuma kama mtumwa, mkomboe mfanye kama ndugu yako, mpe tahfif kama kweli wewe Mcha Mungu, mwambie usifanye kazi bali saidia, wewe Binaadamu mwenzangu, sina haja ya mimi kukunyanyasa, na kama unaumwa pumzika, na kama huwezi kazi basi chukua mtaji katafute cha kufanya uanze maisha mapya, huko ndio kukuomboa, usidhani utumwa umekwisha, hayo mnayoyafanya katika majumba pia utumwa jitakase Nafsi yako kwa kukaa nao kwa wema hao Binaadamu wenzenu, fikiria ikiwa Mollah kakuweka wewe katika hali kama hiyo ungehisi nini.
Na Mkifanya hivyo sasa hapo Sala zenu ndio kwanza zinaanza kukubaliwa, Na Wakawa wanasimamisha Sala na Kutoa Zaka, Na watekelezao ahadi zao wanapoahidi, usiikere Nafsi nyengine kwa kudanganya, kwani kusema uongo kunakuvua vazi la Ucha Mungu, nafasi ya kumkumbuka Mollah wako unaikumbuka katika kudanganya watu. Na Wavumiliao katika Shida na Dhara, Isije ikawa huna pesa unaacha kusali, yasikupate matatizo ukatoka dini, na wala usije kupata Maradhi ukaona Mollah wako kakuonea, inatakiwa uwe mvumilivu wakati wote hata wakati wa misukosuko ya (Vita)lazima muwe wastahamilivu, isiwe mtu anazuka na kusema sijasilimu chochote sababu watu wanapigwa na Polisi.
Hao ndio walosadikisha Uislam wao, na hao ndio wamchao Mungu, na huo ndio Mtihani , basi kama kweli unautaka Ucha Mungu au unadhani ni Mcha Mungu tafuta mambo matatu tu katika hayo, ukiyapata wewe ushasadikisha Uislam wako, lakini fanya kwa ukweli ujue kuwa mimi nimeyapata matatu haya kwa uyakinifu, na hayo matatu yalobakia ndio yatakukamilishia Ucha Mungu wako hususan umo katika Mwezi wa Ramadhan na miezi mengine inayofatia. Mwenye enzi Mungu tupe mapenzi yako tuupate Ucha Mungu, hususan wakati huu tupo karibu sana na wewe, basi tujaalie neema hii ya ucha Mungu ili tuishi kwa Raha Duniani na Akhera.Amin.

Tuesday, July 9, 2013

MALIPO YA TAQWA NI KUSAMEHEWA(QIYYAM LAYLA)PART 1

Asalaam Aleiykum,

Ingia katika Darsa yetu ya leo ili nipate kukujulisha kitu muhimu ambacho kama utakianza leo au kesho kwenye (Yaumu Shaka)basi chaweza kuwa muongozo wa kuupata msingi madhubuti wa hiyo(Taqwa)na ukapata nafasi ya kusamehewa (Dhanmbi)zako katika mwezi huu wa Ramadhan. Sina kipya ninachofundisha ila kukupa upeo mwengine wa kuweza kufahamu njia au mbinu nyengine za kuipata Taqwa.
Pata habari hii ya Ugunduzi wa zama za zamani ulofanywa na wana(Taaluma)wa Sayansi ya utesaji, wanasema hivi, kama utamuashia Taa Mwanaadamu akawa hapati usingizi kwa kipindi cha Mwezi au miezi miwili, basi ataanza kusema yote alotenda, aloyaona na kusikia, iwe  siri ya aina yoyote ama iwe Dhanmbi ilofichika miaka yote, basi atavizungumza vyote na kuvitoa ndani ya kifua chake, kwanza ataanza kimya kimya na siku zikizidi ataanza kutoa sauti kwa nguvu, Na hilo si jambo la kubisha kwani wewe mwenyewe unaweza kuwa kutwa nzima unasema peke yako kichwani mwako, pengine unarejea maneno hayo kwa hayo mara chungu nzima, hayo ndio maafa yanopatikana kwa mateso ya kunyimwa usingizi kwa lazima, na hiyo ni taa walowasha wanaadamu wenzio kwa kukulazimisha, Sasa hebu tupate habari kutoka kwa wanasayansi wa (Kidini)wao wanasemaje kuhusu jambo hili la kuwapo kwa taa, Katika Ulimwengu huu kila kitu kimeumbwa(In Pairs)Adh-Dhaariyat (49).

"وَمِن ڪُلِّ شَىۡءٍ خَلَقۡنَا زَوۡجَيۡنِ لَعَلَّكُمۡ تَذَكَّرُونَ"
"Na katika kila kitu tumeumba dume na jike ili mpate kufahamu"
Wanasema Wanasayansi wa kidini (Mawalii na Wacha Mungu)Na sisi tumegundua hiyo Taa ya pili ambayo inawaka yenyewe ndani ya mwili wako ambayo sikama hii muanayo, hiyo ni (Nuru) na taa hii unaiwasha kwa hiyari yako mwenyewe kwa wingi wa Ibadah na Taqwa, "Kwani hamjasikia kuna kitu kinaitwa Nuru ya Moyo" Sasa nini ufanye mpaka uwashe hiyo (Nuru)?. Mwanzo tumeshaambiwa ukinyimwa usingizi siri na dhanmbi zote zinatoka nje, unatoa mwenyewe habari zote, nini kinafanyika inapowaka hii taa ya moyoni ambayo ni Nuru?.
Sababu tunaingia katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan wacha tuchukue nafasi hii kupeana faida japo kwa uchache ili tupate kuifanya Taqwa kwa ajili ya Mollah wetu, ili na yeye kwa mapenzi yake apate kutusamehe Madhanmbi yetu.Wanasema (Mawalii na Wacha Mungu) kama wao wametumia Sayansi ya nje kuzipata siri zenu, sisi tunakupeni Sayansi ya ndani mpate kusamehewa Dhanmbi zenu. Nini Mfanye, Kasomeni maagizo ya Mollah wenu katika sura ya Muzzamil kuanzia aya ya "1 mpaka aya ya 8" itakutosheni kuiwasha hiyo Nuru. Mollah wenu anakuiteni kwa khiyari yenu mkae macho ili mfanye nini?
Anaambiwa Bwana Mtume s.a.w na sisi sote tunayo tabia hiyo,

"يَـٰٓأَيُّہَا ٱلۡمُزَّمِّلُ" "Ewe uliyejifunika maguo" nguo zinakupa joto joto, ushazizoea, bila ya kujifunika hupati usingizi, sasa unaambiwa ziondoshe, wakati ushafika kama una haja ya kuzungumza na Mollah wako, kama unataraji kuwa karibu na Mollah wako hususan katika mwezi huu wa Ramadhan na miezi mengine, itabidi ufanye jambo hili,"قُمِ ٱلَّيۡلَ إِلَّا قَلِيلاً۬" Simama usiku (Kucha ukifanya Ibada)ila muda kidogo" fanya jitihada ya kuiwasha hiyo (Nuru)kaa macho kwa ajili ya Mollah wako, Sali sana upate kufanikiwa uyapate mapenzi ya Mollah wako, na hayo mapenzi yakupate wewe,
 "Pia napenda uelewe  (Sharaf ya Muumin) ni (Qiyyam Layla) Utukufu wa Muumin ni kisimamo cha usiku," huna haja ya kulala masaa yote, futa madhanmbi yako kwa kuzungumza na Mollah wako sana, usije ukaiwacha nafasi hii ndani ya mwezi wa Ramadhan. Na kama huwezi ufanye nini?
Endelea Part 2.


MALIPO YA TAQWA NI KUSAMEHEWA(QIYYAM LAYLA)PART 2

Asalaam Aleiykum,

" نِّصۡفَهُ ۥۤ أَوِ ٱنقُصۡ مِنۡهُ قَلِيلاً" "(Fanya)Nusu yake au ipunguze kidogo" kama kweli ishakuwa huwezi basi umepewa nafasi usiwache kabisa fanya japo kidogo(ukiwa mgonjwa au unakwenda kazini)                "أَوۡ زِدۡ عَلَيۡهِ وَرَتِّلِ ٱلۡقُرۡءَانَ تَرۡتِيلاً "Au izidishe na soma Quraan vilivyo(Kwa uzuri)basi ikiwa huwezi soma Quraan kwa wingi,
"إِنَّا سَنُلۡقِى عَلَيۡكَ قَوۡلاً۬ ثَقِيلاً"
"Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito" Hii ilokwisha teremka ni kauli nzito iloteremka kutoka kwa Mollah wako, basi fanya hima ujizoeshe kuipitia kila mara kauli hii na utaziona faida zake.
"إِنَّ نَاشِئَةَ ٱلَّيۡلِ هِىَ أَشَدُّ وَطۡـًٔ۬ا وَأَقۡوَمُ قِيلاً"
Hakika (Huko)kuamka usiku na (Kufanya Ibada)kunawafikiana zaidi na moyo, na Maneno (yake)yanatuwa zaidi. Kwanini hapo ukatajwa moyo, umetajwa moyo sababu hiyo Nuru inawaka ndani ya moyo wako na kuenea Mwilini kote, na kutaka kujua hilo wewe mwanzo ukiumbwa kitu cha mwanzo kinachofanya moyo wako upige ni hiyo(The electrical impulse from the SA node triggers a sequence of electrical events in the heart )Sasa ikiwa kumbe kwenye huo moyo wenyewe una umeme kwanini ushindwe kuuwasha ukakuongoza, na umeshaambiwa nyakati za usiku ndio kunawafikiana uzuri, sababu kiza kishaingia na maneno unayozungumza yanateremka kwenda kuiwasha hiyo(Taa) au nuru ya Ucha Mungu, kwa sababu maneno ni (Sound) na hiyo (Sound) karibuni itakuja kugundulika inatokana na (Electric) ndio maana ukaambiwa viwili hivi vinakubaliana,
"إِنَّ لَكَ فِى ٱلنَّہَارِ سَبۡحً۬ا طَوِيلاً۬" 
"Hakika mchana una shughuli nyingi" Usije ukajidanganya utafanya Ibada mchana, huna nafasi hiyo, kuna mambo mengi yamekuzunguka, kama vile kazi au biashara, na mengineyo ya kelele za mpira na fujo za kisiasa, hupati utulivu, subiri watu washalala yatupe maguo yako uzungumze na Mollah wako akufungulie mlango  wa Taqwa.
"وَٱذۡكُرِ ٱسۡمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلۡ إِلَيۡهِ تَبۡتِيلاً۬"
"Na litaje jina la Mollah wako na ujitupe kwake kwa ukweli",
Litaje jina la Mollah wako kwa wingi sana, fanya Dhikiri moyoni mwako mpaka iwe chochote unachotaka kukifanya mwanzo unamtaja Mollah wako, Ikisha jitupe kwake, na maana ya kujitupa(Sio Ulale)ila umtegemee yeye kwa kila jambo, uwe huna mpenzi mwengine ila yeye, iwe fikira zako kila wakati unamfikiri Mollah wako na kumkumbuka, na utakapodumu katika hali hiyo, ikaonekana ama kweli sasa umejitupa kwa Mollah wako, unakijua nini kinatokezea?
Hapo inawaka Nuru ndani ya kifua chako, na dalili za mwanzo utaona kitu kidogo japo cha kufurahisha machozi yana kumiminika kwa hali unayoihisi, huku moyoni unasema kumbe ndio hivi inavokua, jua hapo Nuru ishawaka, na Nuru ikiwaka giza linatoweka, jua likitokeza usiku unaondoka, hapo tena chochote kile unachofanya kinafuta makosa yako, na ushahidi wa hayo sura ya (Hud aya ya 114),
"وَأَقِمِ ٱلصَّلَوٰةَ طَرَفَىِ ٱلنَّہَارِ وَزُلَفً۬ا مِّنَ ٱلَّيۡلِ‌ۚ إِنَّ ٱلۡحَسَنَـٰتِ يُذۡهِبۡنَ ٱلسَّيِّـَٔاتِ‌ۚ ذَٲلِكَ ذِكۡرَىٰ لِلذَّٲكِرِينَ"
Na simamisha Sala katika Ncha mbili za Mchana(Aduhuri na Alasiri) na nyakati za usiku zilizo karibu na Mchana(Nazo ni Magharibi na Isha)Hakika ya Mema huondoa Maovu, Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka. Ukijitupa kwa Mollah wako utakua unakumbuka na ukikumbuka ndio huko kuwasha Taa(Nuru)na taa ikiwaka hutendi maovu ila mema, na huko kusimama usiku kusali na kusoma Quraan ni mema matupu, na hapo ndio inapatikana lile kusudio la (Malipo ya Taqwa kusamehewa).
Ikiwa taa ya nje inatoboa siri zako na dhanmbi zako ulofanya hii 
 Taa ya ndani inapowaka  inafuta dhanmbi zako, na inakufanya unakua (More Alert) ukinyanyuka usiku unavunja uwezo wa kutenda maovu, inateremka moyoni mwako neema hii ya (Taqwa) mpaka inageuka khofu, nini khofu? utashangaa nikikwambia khofu ni mapenzi, na hiyo khofu ni sawasawa na ushujaa, yote ni mapenzi moja penzi la ndani na la pili ni penzi la nje. katika kutafautishwa ndio moja likaitwa khofu na jengine kuitwa ushujaa, anopewa yote mawili anakua mwenye kufuzu, anakua (Shaahid) ndani anamuogopa Mollah wake na nje anajikinga na yale Aloharamisha Mollah wake, huyo kaipata (Taqwa) na huyo ni mwenye kufuzu.
Na nyinyi sasa mshazijua mbinu za kuwasha taa ya Ucha Mungu, na mnaingia katika mwezi wa kujilinda na vyote vilo haramishwa na Mollah wetu, basi zidisha juhudi mpaka ifikie kile cha halali unakiogopa kisije kuwa cha haramu, hiyo pia ni dalili za (Taqwa). Na ukifanya hivyo itakua Taa yako au Nuru uliyoiwasha moyoni  itamurika katika kiza cha Madhanmbi, na huku unaendelea kuomba Maghfira kwa madhanmbi yako yote, Na hiyo ndio faida ya Taqwa.Usisubiri mpaka mtu akuamshe, nyanyuka mwenyewe upate kurehemewa , Nyanyuka usiku upate kusamehewa, simama kucha ulitaje jina la Mollah wako ili upate kunusuriwa na Moto wa Jahannam, Na hayo kwa ufupi ni baadhi ya malipo ya Taqwa.

Friday, July 5, 2013

RAMADHAN:KUFUNGA(SWAUM)NI MAUMBILE PART 1

Asalaam  Aleiykum,

Umekaribia mwezi mtukufu wa Ramadhan na sisi bora tuanze kujiandaa kwa kumkaribisha mgeni wetu huyu kwa unyenyekevu ulio mkubwa kabisa, Wacha tuanze kuzikosha (Roho) zetu kwa maneno yenye nuru, maneno ya Muangaza. Katika darsa hii tutajifunza mambo muhimu ili tupate kuifanya Ramadhan yetu ya mwaka huu iwe tafauti na zote zilopita, fatana na mimi nikushike mkono ili nikuoneshe wito huu wa Mollah wetu unakuelekeza pahala gani, Na kwanini ukaitwa?, Na wewe uloitwa ni nani?.
Katika safari hii kuna mambo yatakuzindua ili upate kujijua kama wewe ni mtu (Special) kwa Mollah wako, Darsa hii madhumuni yake ni kuwasha (Taa) ya (Roho) yako ambayo katika kipindi hiki cha miezi kumi na moja kwa makusudi umeizima, Najua unaweza kushangaa mbona darsa hii tafauti na (Sheikh) wangu, kusudio langu mimi ushangae, Na ukishangaa ndio ushakamata hiyo (Switch)na sasa ushawasha hiyo (Taa).
Sababu tumeshachoka na vigoma vya kuamsha daku, kila tukipiga huamki unazidi kulala(fofofo), unapata darsa hii yenye kufungua na kupenya kwenye (Akili) yako ili upate kujua nini (Funga-Swaum)?na kwanini ufunge?
Nimetanguliza darsa hii kwa sababu kuna watu (Shetani)kashawavamia ili watengeneze maradhi ya kubuni, kuna wanowaza (Ulcer) ndio zinaanza kuchipua magonjwa haya na yale yanaanza kujitokeza katika mwezi huu wa Shaaban, ili itapoingia Ramadhan mtu aendelee kuuchapa (Mpunga)kama kawaida yake.
Leo hapa nataka kueleza nini hasa dhumuni la hiyo funga(Swaum) lakini kabla ya kufanya hivyo hebu tuiangalie (Funga) jee ni kweli (Maumbile)yetu. "Ewe Mwanaadamu amka(Washa Taa) ujue yakwamba wewe unafunga kila siku lakini upo gizani hutambui" Sababu umelala na sasa wacha nikuamshe uone vipi unafunga katika haya masaa (24) ya Uhai wako, "Wewe una dasturi ya kufunga masaa (21) kutokana na (Basic Nature) ya kiwiliwili chako", Nikisema hivyo najua wengine watajiuliza mbona nakula (Chewing gum), mbona navuta Sigara, mbona nakunywa (Juice) na amali zengine unazozifanya mwenyewe ambazo unazijua, zote hizo ukizichunguza ni tabia lakini sio (Basic Nature) yako, Mwili wa binaadamu hautaki ziada ila (Akili) yako ndio yenye kutaka ziada, jitizame unakula ukiwa na njaa au unakula kwa mazoea.
Mwanaadamu unaivunja Ibadah hii ya Swaum kutokana zile nyakati unazokula unakua pia umetawaliwa na mazungumzo pengine ya siasa, au unakula huku unazungumzia Mpira, au sherehe za harusi ndio zimetanda wakati wa kula, Chakula hukipi heshima yake, unasahau chakula kimetokea wapi hata kukufikia wewe  mezani kwako, unasahau Nani alokitia Ladha, Nani alokifanya kiwe kitamu, jiangalie vipi unakula utaona unatupa kapuni, hujui hata ladha ya chakula, unakula bila ya njaa, unakula kwa kufata tabia, imefika saa saba ni (time) ya kula, hata ikiwa huna njaa wewe unakula, hata iwe nusu saa ilopita ushapiga bakuli la (Urojo).lakini hukubali na ugali lazima utie kapuni.
Lakini ikiwa utakula kwa kufata mwito wa Njaa basi utagundua kila siku ya maisha yako ni (Swaum) kwako, vipi inakua hiyo Funga.
Endelea Part 2

RAMADHAN:KUFUNGA (SWAUM) NI MAUMBILE PART 2

Asalaam Aleiykum,


Sasa tizama kama utafata utaratibu ulopangiwa wa kula inapokushika njaa vipi itakua (Swaum) yako. Tuseme unaanza kula saa mbili asubuhi ukala na kukipa heshima na adabu zake zote  chakula, Basi Mja wewe una uwezo wa kutokula mpaka saa nane ya mchana(Umepata masaa 6)unamaliza kula saa (8) mchana huli tena mpaka saa (1) usiku, na ukimaliza hapo huli tena usiku kucha mpaka alfajiri yake, usishtuke funga zipo za aina nyingi na hizo ni (Sunna)zilokubalika zengine zinajulikana zengine zimefichikana na moja wapo katika hizo ni ile ya (Bibi Maryam) alipoambiwa katika sura ya (Maryam) aya ya 26"
"فَكُلِى وَٱشۡرَبِى وَقَرِّى عَيۡنً۬ا‌ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ ٱلۡبَشَرِ أَحَدً۬ا فَقُولِىٓ إِنِّى نَذَرۡتُ لِلرَّحۡمَـٰنِ صَوۡمً۬ا فَلَنۡ أُڪَلِّمَ ٱلۡيَوۡمَ إِنسِيًّ۬ا"
"Basi ule na unywe litue jicho lako(Furahi) Na kama ukimuona mtu yoyote(Akauliza habari ya mtoto huyu) Sema, hakika mimi nimeweka nadhiri (Kwa Mwenye enzi Mungu)Mwingi wa Rehma ya kufunga, kwa hivyo leo sitosema na mtu"
Naam hiyo ndio faida ya kula na kunywa , ikishe utulie ufurahi sasa ushashiba, sio tena ukipita ule hichi halafu ule kile wacha tabia ya (ulafi) weka (Balance) na mtu akikukaribisha mwambie mie nimefunga sili tena mpaka usiku, zote hizo ni (nadhiri) na kufanya hivyo kutakupelekea saa zote kumkumbuka Mollah wako, jaribu japo wiki utaona raha yake, utaona wapi unaelekea, Na ukiweza kufanya hivyo ukawa unakumbuka kwa muda wa miezi mitatu tu itakujia fahamu yakujua ama funga ndio (Nature) yangu, na kuanzia siku hiyo ikikujia fahamu hiyo utaweza kuupata (Ucha Mungu) na kuweza ku(Control)tabia yako, na wala hali hiyo haitokutoka tena, kumbuka (Funga)ni Maumbile yako, maisha yote wewe uko katika (Swaum)lakini sahau tu ndio ilo kushika na umezongwa na maisha na mambo mengine mengi takriban miezi kumi na moja, Sasa Ramadhan imeletwa kwa ajili gani?.
Katika mwezi wa Ramadhan unapatikana huo (muamsho) au wito maalum kwa Waumin kuitwa na Mollah wao watoke katika kusahau, katika kipindi hiki sasa wawashe taa na kuijua faida ya hii (Funga)"Al Baqarah 183"

"يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡڪُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِڪُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ"
"Enyi Mloamini mmelazimishwa kufunga kama walivo lazimishwa waliokua kabla yenu ili mpate kumcha Mungu"
Sasa nini kinatokea kwa Muumin mwenye kuukubali wito huu, "Enyi Mloamini wito huu ni (Special) kwenu nyinyi waja wangu kujijua nyinyi ni nani na mko hapa kwa madhumuni gani, miezi 11 yote mmeshughulika na Biashara au Siasa, mmeshughulika na mambo ya Ofisi au Maharusi na mengineyo, Mwezi huu mnatakiwa katika siku hizi chache kama nyinyi Waumin wa kweli basi sahauni kila kitu, Ikisha mfanye nini? Jitafautisheni na hicho kiwiliwili(Body) juweni nyinyi ni muungano wa vitu viwili (Ardhi) Kiwiliwili na hicho cha pili ni hiyo (Roho) na hii Ramadhan ndio hiyo Ustaadh wa kuilea hiyo (Roho) Vipi italelewa hiyo Roho?
Katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhan, tumo katika kufanya uchambuzi wa (Swaum) kwa njia ya (Tawhid) naomba mnistahamilie ili twende kidogo kidogo upate kuifahamu" 
" كُتِبَ عَلَيۡڪُمُ ٱلصِّيَامُ"
Sasa nakuamrisheni kufunga, Nini kufunga? Kufunga ni Maumbile yenu, siku za kawaida mnafunga bila ya kujifahamu, bila ya kukumbuka mefunga, ila mwezi huu mmeamrishwa mkumbuke, nini kinafanyika hapo, hayo masaa matatu niloyataja mwanzoni mnayo kula na kunywa, moja linaondoshwa na yale mawili yalobaki yanabadilishwa mwenendo kutoka mchana kwenda usiku
" ثُمَّ أَتِمُّواْ ٱلصِّيَامَ إِلَى ٱلَّيۡلِ‌ۚ"
"Ikisha itimizeni Swaum mpaka usiku"
Nini kinatokezea, wewe chunguza (Mwili au Body) inaponyimwa chakula kinapatikana kitu (Awareness) Ufahamu, au kukumbuka au (Dhikr) ikipatikana fahamu hii sasa Waumin wanaitumiaje?
Endelea part 3

RAMADHAN:KUFUNGA (SWAUM)NI MAUMBILE PART 3

Asalaam Aleiykum,

Kuna wengine wanaitumia fahamu hii kwa kucheza karata, wengine wanatumia kwa kucheza bao au kutizama senema au na kujishughulisha na harakati zengine ili wapate kujizubaisha na hii (Awareness)kumbukumbu ilowashukia, wanasema poteza muda ili masaa yaende, kumbe hapo wanakosa kitu adhimu kabisa cha kuzungumza kwanza na Mwili wako, habari za siku nyingi, tulikua tumegandana hata ukanisahau, mimi naitwa kiwiliwili na sasa nina njaa, mwenzio taabani, hivi sasa nina hamu ya maji, ukipata fahamu kama hii ushaweza kujitenga na kiwiliwili, sasa unajua kumbe anosikia njaa ni kiwiliwili(Body) mimi ninayefahamu kuwa kiwiliwili kina njaa ni nani?, hapo inakua ushapata (Separation) na hiyo (Separation) ndio kusudio la (Funga) na hapo inakua (Taa) ishawaka unaanza safari ya kwenda huko kwenye (Taqwa). Hapo inatakiwa uigeuze (Fahamu) hiyo sio kwa mambo nilotaja hapo juu, badala ya kucheza karata elekeza mawazo yako katika kipindi hicho kusoma Quraan sana, Badala ya kucheza Bao Sali sana, badala ya kutizama Tv kaa umkumbuke Mollah wako akufungulie Fahamu zaidi, badala ya kujizubaisha Mkumbuke Mollah wako kwa kumsabihi na kumtaja kwa majina yake na ujitahidi uyajue na maana yake, fanya hima vitendo vyako vyote viwe vya kheri na hiyo ndio maana ya "Kama walopita kabla yenu ili Kumcha Mungu"
Na hapa ndio unapata Fahamu ya kujua kumbe katika mwezi huu wa Ramadhan kuna vitu viwili muhimu nimevijua na lazima nivipate, cha kwanza ni hiyo (Swaum) ita unavopenda, kuwaka kwa (Taa)ita (Awareness)ita(Fahamu)ama(Kukumbuka-Dhikr) lakini dhumuni lake ni hilo la (Muamsho). Napenda vilevile ufahamu tafauti yako wewe Muumin na Mcha Mungu ni hiyo (Taa)au(Hadhir)au(Awareness) Muumin yeye anazima na kuwasha, Mcha Mungu inakua imewaka wakati wote, Ndio kwenye mwezi huu wa Ramadhan mnaitwa sasa washeni moja kwa moja, na (Taa) ikiwaka kikweli Shetani haonekani, hapo utastaajabu kwanini Taa imewaka na Shetani haonekani, Sababu Shetani ni mwizi hakai kwenye nuru(Anafungwa)gizani.
Ndio maana utaona ukishawasha hiyo (Switch)(Energy)inatumika pahala pengine, unakua hutamani (Sex)na kila kitu kinakatika, na kikubwa mtu anageuza Fahamu yake yote katika chakula, kila kitu anaona hakitoshi, kashughulika mtu atakula nini (Magaharib)lau angepata kumkumbuka Mollah wake Badala ya chakula mja huyu daraja yake ingekua ya aina nyengine katika mwezi huu wa Ramadhan. Angejua Mawazo yote alokua nayo angeyageuza katika hiyo Taqwa, na asingekumbuka (Makalmati na vyakula vyengine) ila angekua Mwenye kufanya (Itiqaf)au(Sala)au(Kusoma Quraan) na kila ukizidisha vitatu hivyo katika mwezi huu na daraja yako inapanda, Na ukibahatika kufika kileleni ndio unaipata hiyo inayoitwa(Lailatul-Qadir) Umeshapanda kwa Mollah wako na ukiupata usiku huo ndio Malaika wakiteremka na Roho yako unakua ushabadilika, unakua kiumbe mwengine kabisa, na hiyo ndio Maana ya "Bora kuliko miezi elfu" au miaka yako yote 83 ikiwa utaishi, ukiupata usiku huu unatakasika na unakua(Pure) hiyo ndio faida ya (Taqwa)iliyotimia, lakini kumbuka ina vishindo kufikia hali hiyo, hautakiwi uzembe wala uvivu, unatakiwa uwe safi kuanzia Macho,Akili, mpaka chakula chako kinachokwenda ndani ya kiwiliwili. Ikisha ukumbuke " أَيَّامً۬ا مَّعۡدُودَٲتٍ۬‌ۚ" "Ni siku chache"(Kidogo) "Ewe" Mwanaadamu wewe umepewa uhai na ukapewa maisha haya ya dunia na vyote ulivonayo, basi Amri hii ya siku kidogo inakushinda, unaona dhiki kwa ajili ya kufunga, huoni fakhari wewe kutii amri ya Mollah wako, Mbona (Boss) wako kazini unamtii amri zake, Basi ikiwa umezinduka ifanye Ramadhan ya mwaka huu iwe umeitwa na Mollah wako na wewe unatii wito wake, kwa furaha na mapenzi na huo ndio mwanzo wa Taqwa.

" فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوۡ عَلَىٰ سَفَرٍ۬ فَعِدَّةٌ۬ مِّنۡ أَيَّامٍ أُخَرَ‌ۚ وَعَلَى ٱلَّذِينَ يُطِيقُونَهُ ۥ فِدۡيَةٌ۬ طَعَامُ مِسۡكِينٍ۬‌ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيۡرً۬ا فَهُوَ خَيۡرٌ۬ لَّهُ ۥ‌ۚ وَأَن تَصُومُواْ خَيۡرٌ۬ لَّڪُمۡ‌ۖ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ"
"Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari(Akala mchana)basi (atimize)hisabu katika siku nyengine, Na wale wasoweza watoe fidia kwa kumlisha maskini, na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake, Na kufunga ni bora kwenu, ikiwa mnajua".
Na hiyo Swaum ni kheri kwenu ikiwa mnatambua, Sasa zigundue kheri mbili za Swaum, ya kwanza ni (Cure)Matibabu inaponesha maradhi mengi katika kiwiliwili cha mwanaadamu, Na jambo la pili unapata hiyo (Pureness of the Soul) unapata (Taqwa) hizo ndizo kheri mbili zipatikanazo katika funga ya Ramadhan, kupona kwa maradhi na kutakasika kwa Roho nayo ni hiyo Taqwa.
Tunakuomba Mollah wetu zikubali nia zetu, uzikubali funga zetu, uturidhie tuupate Ucha Mungu, sio kwa mwezi huu wa Ramadhan tu bali hadi mwisho wa uhai wetu. Amin.