Sunday, July 14, 2013

MTIHANI WA TAQWA PART 4

Asalaam Aleiykum,

"وَأَمَّا مَنۡ أُوتِىَ كِتَـٰبَهُ ۥ بِشِمَالِهِۦ فَيَقُولُ يَـٰلَيۡتَنِى لَمۡ أُوتَ كِتَـٰبِيَهۡ"
Lakini atakayepewa daftari(Kitabu)lake katika mkono wake wa kushoto basi yeye atasema (Bora)Laiti nisingelipewa daftari langu.
Unaangalia Kitabu sifuri tupu, unaona leo nitakiona cha mtemakuni.
Kuamini Manabii wake(5)?(Fumba macho) Hujawahi kuwaona wala kuwasikia vipi utaamini, hapo unamrejea Mollah wako akupe huo muongozo wa kuwaamini na kuwakubali Manabii wake, kutokana na ishara na athari walizoziacha, kutokana na maneno waliyoyaleta, na habari zao unazosomewa, halafu jifanyie mtihani ndani ya nafsi yako, hivo kweli Mtume s.a.w angekuwepo leo ningemkubali, mbona likitajwa jina lake sihisi kitu, mbona damu hainichemki, jee angekuwepo Nabii Isa a.s (Jesus) akanambia mtu akikupiga kibao mgeuzie upande wa pili ningekubali, vipi ningekutana na Nabii Musa a.s akanambia pita katika bahari ningemfata, ukipata majawabu hayo utajua nini Imani yako kuhusu Manabii.
Sasa wacha tuingie katika Barafu ya Moyo, wacha tuguse tuone vipi watu wanavoichukia Dini, tizama wangapi watazima Computer, kuna watofikia mpaka kutukana, kwanini, sababu tunagusa yanayowashinda wengi kutekeleza nayo ni hiyoo Mali, hiyo ndio Fitna ya mtu kukubali kuikosa Taqwa lakini abakie na Mali.
Na Wanawapa Mali(6)?(Funga Macho) Jiulize unatoa wewe Mali yako, huo Mtihani mkubwa, na mwanzo unaambiwa ile unayoipenda ndio itoke mwanzo, Una nyumba tatu, ile Flat ya Upanga unamtafuta ndugu yako wa karibu, hii chukua wewe, una Nyumba Baharini Mangapwani unamtafuta jamaa yako wa karibu wewe huna kitu hii chukua wewe, una gari mbili wewe za nini, na hupandi zote itoe kwa jamaa zako wa karibu, una mkufu wako wa dhahabu mpelekee jamaa yako huu shika wewe, maskini hamna hata pesa ya futari nendeni kauzeni ili mpate chakula, huo ndio ucha Mungu, Jee wewe unafanya hayo, Una mapesa Bank yamelaliana nje kuna Mayatima wangapi unatoa kwa ajili yao, Unawapa wewe Maskini, Mtu kakufata kaharibikiwa hana tiketi ya kurudi nyumbani jee unampa, anakuomba nauli unamfonya halafu unajiita Mcha Mungu, na wale wanoomba ukawapuuza yote ni mitihani Mollah anakuletea, anatumwa Muombaji aje kwako kwa kusudi, na wewe jitizame sasa umepata wasiwasi, eti wewe ndio unakimbia usiombwe, Na katika kuwakomboa Watumwa, Na kumkomboa Mtumwa sio lazima awe kanunuliwa, yumo umemuajiri mfanyakazi wa nyumbani, unamtuma kama mtumwa, mkomboe mfanye kama ndugu yako, mpe tahfif kama kweli wewe Mcha Mungu, mwambie usifanye kazi bali saidia, wewe Binaadamu mwenzangu, sina haja ya mimi kukunyanyasa, na kama unaumwa pumzika, na kama huwezi kazi basi chukua mtaji katafute cha kufanya uanze maisha mapya, huko ndio kukuomboa, usidhani utumwa umekwisha, hayo mnayoyafanya katika majumba pia utumwa jitakase Nafsi yako kwa kukaa nao kwa wema hao Binaadamu wenzenu, fikiria ikiwa Mollah kakuweka wewe katika hali kama hiyo ungehisi nini.
Na Mkifanya hivyo sasa hapo Sala zenu ndio kwanza zinaanza kukubaliwa, Na Wakawa wanasimamisha Sala na Kutoa Zaka, Na watekelezao ahadi zao wanapoahidi, usiikere Nafsi nyengine kwa kudanganya, kwani kusema uongo kunakuvua vazi la Ucha Mungu, nafasi ya kumkumbuka Mollah wako unaikumbuka katika kudanganya watu. Na Wavumiliao katika Shida na Dhara, Isije ikawa huna pesa unaacha kusali, yasikupate matatizo ukatoka dini, na wala usije kupata Maradhi ukaona Mollah wako kakuonea, inatakiwa uwe mvumilivu wakati wote hata wakati wa misukosuko ya (Vita)lazima muwe wastahamilivu, isiwe mtu anazuka na kusema sijasilimu chochote sababu watu wanapigwa na Polisi.
Hao ndio walosadikisha Uislam wao, na hao ndio wamchao Mungu, na huo ndio Mtihani , basi kama kweli unautaka Ucha Mungu au unadhani ni Mcha Mungu tafuta mambo matatu tu katika hayo, ukiyapata wewe ushasadikisha Uislam wako, lakini fanya kwa ukweli ujue kuwa mimi nimeyapata matatu haya kwa uyakinifu, na hayo matatu yalobakia ndio yatakukamilishia Ucha Mungu wako hususan umo katika Mwezi wa Ramadhan na miezi mengine inayofatia. Mwenye enzi Mungu tupe mapenzi yako tuupate Ucha Mungu, hususan wakati huu tupo karibu sana na wewe, basi tujaalie neema hii ya ucha Mungu ili tuishi kwa Raha Duniani na Akhera.Amin.

No comments:

Post a Comment