Saturday, July 27, 2013

WAJUE WALOFUNGA MWAKA HUU PART 3

Asalaam Aleiykum,

Watu wengi inapofika katika kufanya Taqwa wanakua hawajui nini hasa msingi wa Taqwa, Mti huu wa Taqwa una matawi mengi madogo madogo, kama vile kutoa sadaka, kuhurumia wazee na wagonjwa, kutoa zaka na  matawi mengi mengine, lakini inapofika katika mti wenyewe watu wanaganda hawajui wafanye nini, mtu hana mashiko wala dalili, haelewi vipi afanye aipate hiyo zawadi kubwa ya mapenzi ya Allah, vipi atakutana na kile kisicho onekana, afanye nini atosheleze nafsi yake ili ajue ama kweli mimi nimepata (Contact) na (Beyond), Sasa leo mtaniwia Radhi ili nikuchukueni kwenye hii safari japo nusu njia ili nikuoneshe vipi utapata hiyo Taqwa ya Mwenye enzi Mungu, ambayo katika mwezi huu ni kusudio lenyewe, igundue siri ya wanofunga na kufanya Taqwa wanakua katika hali gani kwenye mwezi huu ili na wewe ujiunge nao.
Nipeni ruhusa nizungumze sura ya Al-Imran aya ya 190 mpaka 191, ili tupate kugundua hiyo Taqwa ikoje na vipi ukurubie kwa Mollah 
wako,
 "إِنَّ فِى خَلۡقِ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ وَٱخۡتِلَـٰفِ ٱلَّيۡلِ وَٱلنَّہَارِ لَأَيَـٰتٍ۬ لِّأُوْلِى ٱلۡأَلۡبَـٰبِ"
"Katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutafautiana (baina)ya usiku na Mchana, kuna alama (Ya kuwapo Mwenye enzi Mungu) kwa wenye Akili".
kwanini ikatajwa Mbingu kuumbwa kwake na wewe hujaishuhudia, sababu katika Mbingu ziko alama, na sasa mnasomeshwa, ukizitizama mwenyewe nyota unaona zinakwenda, kuna nyota zile tano zinoonesha pembe zote za Ulimwengu huu, kuna mambo ya kila aina huko juu, lakini mchana hatuyaoni tumefunikwa na hii taa ingarayo kwa mwanga mkali, na katika hii ardhi, ukiwa mcha Mungu wa kweli utaona mambo ya ajabu ya kila aina, kuna alama kwa Mabilioni zimetuzunguka, lakini wengi hatutumii akili hata wakati huu wa Swaum ambapo akili imetulia na inaweza kugundua mambo mengi, hebu angalia vipi maisha yalivo, tizama wanyama kila mtu alivopangiwa shughuli zake, Ndege ana mambo yake, vidudu vina mambo yao, paka ana mambo yake, mpaka kuku ana shughuli zake za pekee, na wanaadamu hali kadhalika kila mmoja ana fikra zake na matendo yake, ikisha kuyaona hayo, halafu tizama sote tulivo pewa uhai, sote tukawa tunaishi kwa amri yake Ikiwa Mcha Mungu au umepata Swaum kikweli basi utaangusha macho chini ikisha useme kwa hilo Mollah wangu nathibitisha kuwepo kwako pasipo na shaka yoyote, na pia nasadikisha hili halipati yoyote yule alojaza kichwani mwake mambo  chungu nzima ya kidunia katika mwezi  Mtukufu wa Ramadhan.

"ٱلَّذِينَ يَذۡكُرُونَ ٱللَّهَ قِيَـٰمً۬ا وَقُعُودً۬ا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمۡ وَيَتَفَڪَّرُونَ فِى خَلۡقِ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ رَبَّنَا مَا خَلَقۡتَ هَـٰذَا بَـٰطِلاً۬ سُبۡحَـٰنَكَ فَقِنَا عَذَابَ ٱلنَّارِ "
"Ambao humkumbuka Mwenye enzi Mungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala, Na hutafakari umbo la mbingu na ardhi,(Na wakasema)Mollah wetu hukuviumba hivi bure, Utukufu ni wako, basi tuepushe na adhabu ya moto"
Linapotajwa neno kukumbuka watu wengi wanadhani ni ile (dhikr) walizozisikia za kwenye (Mazawiya na zinazofanyika mashamba) hapo kukumbuka sio kusudio hilo, kusudio la hapo ni kukumbuka kwa Mcha Mungu, na wewe umo kwenye mwezi wa Ramadhan unafanya Taqwa, basi ipate maana ya kukumbuka huko, ili hizo siku kumi zilobaki uwemo katika kundi la walofunga, Kukumbuka kuliko kusudiwa hapa ni kule kila saa na dakika, hususan kwenye mwezi huu wa Ramadhan, hebu pata maana ya neno Muabudu Mollah wako kama unamuona, lina maanisha uwe unajua popote ulipo uwe unafahamu Mollah wako pia ni mwenye kukuona, chochote ukifanyacho uwe unatambua Mollah wako ni mwenye kushuhudia,Ukikaa kitako ukamuona kipepeo anaruka,  uwe unaziona alama za Mollah wako, vitoto vinacheza ukumbuke na wewe uliwahi kuwa kama wao na sasa Mollah wako kakufanya umekuwa mkubwa kwa malezi yake,Mshipa wa swaum ukikushika ukataka kulala usikumbuke maandazi na machopo chopo, ila mkumbuke Mollah ana kujulisha mshipa wa Swaum na kukuangalia mja wake, ukikaa na wenzio wao wanacheka wewe mkumbuke Mollah wako useme,Mollah wangu nikurubishe kwenye Ufalme wako , unifanye kuwa kipenzi chako, Usininyime mimi ladha ya hata dakika moja kuto kukumbuka wewe Mollah wangu,nipe mie uwezo wa kukumbuka nikiwa kazini, nikiwa barazani, nikiwa popote pale ambako waja wako wamekusahau, basi naomba hii hadhi ya Ucha Mungu initeremkie niwe na sifa ya kukumbuka, na pia uwe unatambua Mollah wako anazungumza na wewe kwa lugha mnayofahamiana, mfano kama vile anavo kunusuru na mabalaa na unajua kuna kitu ndani ya hisia zako kimekwambia leo usende pahala fulani, au unasema Roho yangu nzito, halafu unasikia ahh imetokea ajali watu wamejeruhiwa vibaya sana, baada ya kugundua umezungumza na Mollah wako, unazuka na kusema (Machale yamekucheza) au ukinusuriwa na dhuluma au kuibiwa unasema umecheza kama Pele, unaonesha jinsi gani ulivomsahau Mollah wako. Ila unamkumbuka wakati mmoja tu unapotaka kuomba au ukiwa unaumwa, hapo dua na Sala zitatumwa na machozi, lakini nyakati zote humjui kabisa na yanakutoka hata kama umeumbwa.
Basi husema wale wenye kuishika Taqwa na kuipata Swaum, Ya Raab hakika hukuumba haya bure tu ndio iwe basi, Hakika umetukuka Mollah wetu basi na sisi tumo kwenye Swaum, na Hili linaloingia ni kumi la dhamana ya kuepushwa na Moto, basi na sisi tunakuomba utunusuru na Moto wa Jahannam.
Endelea part 4

No comments:

Post a Comment