Sunday, September 29, 2013

UZURI WA MAISHA PART 4

Asalaam Aleiykum

 وَلَسَوۡفَ يُعۡطِيكَ رَبُّكَ فَتَرۡضَىٰٓ 
"Na Mollah wako atakupa mpaka uridhike"
Wengi katika sisi tunapewa mpaka tunaridhika, mwanzo ulikua huna familia, Mollah kakukutanisha na Mkeo mmepata kizazi, kakunyanyua maisha umepata uwezo wa kujenga, umemaliza masomo umepata kazi nzuri, una marafiki wapenzi, umezungukwa na familia, umepata cheo katika jamii na kazini, vipi leo unakataa kuridhika, vipi unaona maisha haya ya tafrani, lazima wewe ndio una matatizo lakini sio maisha abadan,kuyaona maisha haya uzuri wake kinachotakiwa Ridhika, kila jambo lako litakua zuri.
 أَلَمۡ يَجِدۡكَ يَتِيمً۬ا فَـَٔاوَىٰ 
"Je hakukuta yatima akakupa makaazi"
Ili uwe shahidi ya hayo katika mpito wa maisha unakumbushwa kutokana na mwenendo wa maisha ya Binaadamu hilo linatokea kila leo, la wazee mmoja au mwengine kufariki na Mtu kulelewa na watu wengine, kwa hiyo kuoneshwa Uzuri wa maisha haya unapokuja kwenye Ulimwengu huu basi unapewa makaazi ya kuhifadhiwa, na kama walivofanyiwa wengi walopoteza wazee wao, na taratibu hii inaendelea mpaka hivi sasa.
وَوَجَدَكَ ضَآلاًّ۬ فَهَدَىٰ
"Akakukuta umepotea(Hujui cha kufanya)akakuongoza"
Sote tunafikwa na hali hii katika maisha haya, kuna baadhi wanazama kwenye uharibifu ikisha wanaletewa uongofu utokao kwake wakaja kuwa watu wema, hukuongoza Mollah wako katika kufanya mema na kuyaepuka mabaya, hukuachisha kufanya maovu ukawa ni mwenye kutenda Ibadah, na kila mmoja humteremkia uongozi huu na mtu ana khiyari yake kufata au kutokufata.
وَوَجَدَكَ عَآٮِٕلاً۬ فَأَغۡنَىٰ
"Na akakukuta maskini akakutajirisha"
hakuna anozaliwa tajiri, sote tunatokea katika hali duni, ikisha Mollah wetu anatupa kwa taratibu alotupangia mwenyewe mpaka tukaridhika, isipokua wale wanoamua kuchukuwa wenyewe kwa njia za mabavu, rushwa na mengineyo hao kawapangia malipo yake katika maisha haya.
فَأَمَّا ٱلۡيَتِيمَ فَلَا تَقۡهَرۡ 
"Basi usimuonee yatima"
Ukaona huyu hana msaidizi wacha ni mdhulumu, au kumnyanyasa, usiharibu mwenendo huu wa maisha mazuri kwa kumfanyia yatima uzito na dhuluma, kumbuka yuko alo juu yako na yeye atakuonea kama unavoonea.
 وَأَمَّا ٱلسَّآٮِٕلَ فَلَا تَنۡہَرۡ 
"Na wala usimkaripie aombae"
Mpaka mtu akaja kwako kukuomba ujue ana shida kwa hali unayoijua, basi hata kama huna mjibu kwa unenyenyekevu, na kama unacho usizuie mpe japo kidogo, ili huzuni iondoke moyoni kuwa umemnyima, wewe utafarijika na yeye atapata faraja, na huo ndio uzuri wa maisha. 
 وَأَمَّا بِنِعۡمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثۡ
"Na Neema ya Mollah wako hadithia"
Sasa ushakua na fahamu, ushaishi maisha haya na umeyaona mengi katika mambo ni mazuri kuliko mabaya, umeridhika na ulichonacho, umejaaliwa kutembea hapa na pale, umefika huku na kule, umekutana na huyu na yule, umeonja hiki na kile, kuna siku umefurahi na siku umelia, kuna muda ulikua na maradhi sasa umepona, yote hayo wewe ni shahidi umeyapitia na unaendelea kuishi nayo, basi ona uzuri wa maisha Mbingu Buluu, bahari shuwari, usiku unaingia, mchana unangara, unavuta pumzi bila ya matatizo, huna tatizo lolote wewe na familia yako, unapata kula yako, pengine (Bank)pesa zimetulia, unafanya ibada kwa utulivu, watoto wanasoma hawana shida yoyote, hizo zote ni Neema za Maisha Mazuri, na inatakiwa uzihadithie kwa mdomo na vitendo ili upate kuona uzuri wa maisha. 
Mollah tujaalie kuona Uzuri wa maisha haya ili tusipate dhiki na uchovu wa kutoamini Maisha hayo yajayo ya Akhera. Amin.


No comments:

Post a Comment