Asalaam Aleiykum,
Ama Mwenye kukufuru "Ambaye kapewa hiyo hekima" akaanza kuitumia vyengine, akaanza kuleta ujanja ujanja, ukweli akauchanganya na uongo, basi atamkuta Mollah hana haja na Mtu huyo, Na ukitaka kumjua Mwenye hekima aliye mkweli utaangalia matendo yake yeye si mwenye kulazimisha jambo,na wala hatoi ushauri. Nini maana ya ushauri? Ushauri ni kitu huna uhakika nacho kitafaa au hakifai jaribuni, hiyo ndio maana ya kushauri, lakini hekima anatoa nasaha kwa kuwa yeye anaelewa jambo kwa uhakika, ndio maana utaona aya inofatia ya (13)Luqman anasema.
وَإِذۡ قَالَ لُقۡمَـٰنُ لِٱبۡنِهِۦ وَهُوَ يَعِظُهُ ۥ يَـٰبُنَىَّ لَا تُشۡرِكۡ بِٱللَّهِۖ إِنَّ ٱلشِّرۡكَ لَظُلۡمٌ عَظِيمٌ۬
Na Luqman alipomwambia mwanawe, Hali ya kuwa anampa Nasiha, Ewe Mwanangu usimshirikishe Mwenye enzi Mungu, maana kushirikisha ni dhuluma kubwa.
Jambo la mwanzo mwenye hekima katika ngazi hii analolijua ni (Shirk)ya aina yoyote ile kuwa ni dhulma kubwa, na Mti wa (Shirk)ni mkubwa ndio maana akmwambia mwanawe kwa tendo la kuelewa ewe mwanangu usimshirikishe Mollah wako kwa chochote kile, vipi leo unamshirikisha yule ambaye kakuumba wewe na vyote vilivyomo kwenye Ulimwengu huu, sijui unamtegemea (Boss)wako, kama si fulani nisingepata kitu fulani, hivi na vile, umekamata matawi chungu nzima ya shirk, basi kitu cha mwanzo usimshrikishe Mollah wako na chochote, na ukiona humshirikishi Mollah wako na chochote basi jua hekima ishaanaza kuteremka.
Utafikri wewe vipi yule aliyeumba mbingu na Ardhi awe na mshirika hapa Ardhini, vipi leo uwe unaamini Shetani na Mizimu ndio ilokufanya ufanikiwe, ukiwa katika Imani hizo jua bado hekima haijafika kwako, Na wala haitofika.
Kwa hiyo utagundua Mwenye Hekima ni mwenye kumtegemea Mollah wake kwa mambo yake yote, (Kumbuka na wewe upo ngazi ya 5, na hiyo tano ukiiwekea Sifuri nyuma inageuka kuwa 50)huo labda ndio Umri wako pengine ndio wakati wa kuzipata hizo Hekima, Luqman anamuusia mwanawe , hekima inatoka kwa mtu mzima kwenda kwa mtoto "Ewe"Mwanangu.
يَـٰبُنَىَّ إِنَّہَآ إِن تَكُ مِثۡقَالَ حَبَّةٍ۬ مِّنۡ خَرۡدَلٍ۬ فَتَكُن فِى صَخۡرَةٍ أَوۡ فِى ٱلسَّمَـٰوَٲتِ أَوۡ فِى ٱلۡأَرۡضِ يَأۡتِ بِہَا ٱللَّهُۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ۬
Ewe Mwanangu kwa hakika jambo lolote lile ijapokua na uzito wa chembe ya hardali(Atom)likawa ndani ya jabali, au mbinguni au katika ardhi, Mwenye Enzi Mungu atalileta(Amlipe alofanya)bila shaka Mwenye enzi Mungu ni mjuzi wa mambo yalofichikana, na mambo yalo dhahiri.
Na ukitaka ujue chochote kidogo katika thamani ya Hekima wewe jitizame kwa siku unasema uongo mara ngapi japo wa kipuuzi, ukiona husemi hata mara moja basi jijue ushajisafishia njia ya kuipata hekima. Na kuna mtihani mwengine mwepesi ukitaka kumjua miongoni mwenu kama yupo mwenye Hekima, tizama kama mpo kwenye chakula nyote mkimaliza utasikia mnasema tumeshiba, lakini mwenye hekima atanyanyuka na kusema chakula kitamu, tizama tafauti yake ya maneno hapo.
يَـٰبُنَىَّ أَقِمِ ٱلصَّلَوٰةَ وَأۡمُرۡ بِٱلۡمَعۡرُوفِ وَٱنۡهَ عَنِ ٱلۡمُنكَرِ وَٱصۡبِرۡ عَلَىٰ مَآ أَصَابَكَۖ إِنَّ ذَٲلِكَ مِنۡ عَزۡمِ ٱلۡأُمُورِ
Ewe Mwanangu Simamisha Sala na uamrishe Mema, Na ukataze mabaya, na usubiri yale yatakayo kusibu, hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki kuadhimiwa.
Ewe Mja usidhani kwamba unasimamisha Sala hakitokufika kitu, uko katika Ulimwengu huu kumbuka uwe tayari kwa chochote kitachokufika, kiridhie na ukikiridhia (Ushakwenda)(Beyond)hakikugusi tena, kitagusa mwili wako, kitagusa akili yako, lakini hakikugusi wewe abadan, ukiligundua hilo basi wewe una hekima, ukilijua hilo basi wewe unaishi ndani ya hekima, Na ukiwa katika hiyo hekima basi sasa anza kuamrisha mema na kukataza mabaya, Na ukiitaka hekima ikufike sawa sawa basi Ewe Mwanangu.
وَلَا تُصَعِّرۡ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمۡشِ فِى ٱلۡأَرۡضِ مَرَحًاۖ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخۡتَالٍ۬ فَخُورٍ۬
Wala usiwatizame watu(Kwa Ujeuri wa kuwanyanyulia Pua)kwa upande mmoja wa uso, (Na)Wala usende katika Nchi kwa Maringo, hakika Mwenye Enzi Mungu hampendi kila ajivunae (Mwenye)kujifagharisha.
Huwezi kupewa Hekima ukiwa una jeuri za kuwatizama wenzio kwa kuwageuzia Shingo kwa jeuri na kuwakejeli, Na wala usijione una Utajiri au Elimu, ukaanza jeuri kumbuka utanyimwa Hekima na (Kubakia na cheo cha Babu Jinga). Na wala usitembee ukawa unatingisha Mabega kwa vyeo ulivyo navyo ili watu wajue au waulizane unamjua yule alopita, kwani kwa kufanya hivyo huwi kabisa Mtu wa Mwenye enzi Mungu, hupandi kabisa katika ngazi ya 5, Na Mollah wako si mwenye kupenda wanojifagharisha.
Ewe Mwanangu
وَٱقۡصِدۡ فِى مَشۡيِكَ وَٱغۡضُضۡ مِن صَوۡتِكَۚ إِنَّ أَنكَرَ ٱلۡأَصۡوَٲتِ لَصَوۡتُ ٱلۡحَمِيرِ
Na ushike mwendo wa katikati, na uteremshe sauti yako, bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote.
Shika mwendo wa katikati, usiwe umezama upande mmoja ukawa kila kitu haramu, unarusha mafatwa bila ya hekima yoyote, na wala usizame kwenye maasi, maana yake kuna watu wanatoka kwenye maasi moja kwa moja wanachupia dini, na wanakua wakali wao, wale wote walokuwamo kwenye dini tokea mwanzo hawafai, hawana Ibada, hapa unapewa nasaha zenye Hekima Shika mwendo wa katikati, unaujua mwendo wa katikati ni upi? ni Furaha, katikati ni Hekima, katikati ni (Blissfull). Na wala usiwe unapiga makele ovyo ovyo kama mchiriku, unazuia hata hekima kukushukia kutwa unazungumza, kila siku una hutubia, mazungumzo kwa wingi na makelele chungu nzima kama ya debe. Na unajijua kwanini unapiga makelele sana, jichunguze utagundua ni Tafrani na mambo mengi kichwani, pengine ujinga umezidi, au mgonjwa unataka upige makelele upate nafuu, ndio maana utaona mwenye machungu anapiga kelele, huwezi kuwa na hekima ikiwa litakuwepo zogo kichwani mwako, umepanda ngazi ya tano unatakiwa uwe mpole, uwe karimu, uwe mkimya na hapo tena utaona umeshakuwa Hekima, kila kitu chako kinageuka kuwa hekima na hekima ikitimia unakuwa umeshaaminiwa na Mfalme wa Mbinguni, na ukiaminiwa na Mollah wako unapewa kitu chengine ambacho tutakutana nacho ngazi ya sita. Inshaa Allah wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment